Timu ya watu 7 inayoundwa na wataalamu wa afya kutoka Chama cha Msalaba Mwekundu cha China imeondoka leo, ikiwa na vifaa vya matibabu kuelekea Italia, nchi inayokabiliwa na hali mbaya ya maambukizi ya virusi vya korona (COVID-19). Hadi kufikia jana jioni, jumla ya wagonjwa zaidi ya elfu 12 waliripotiwa kuambukizwa, huku idadi ya vifo ikifikia 827.
Katika wiki 7 zilizopita, China imetumia kila njia katika kukabiliana na maambukizi ya COVID-19, na sasa juhudi hizo zimeanza kupata mafanikio na kuzipatia muda nchi mbalimbali duniani kufanya maandalizi ya kukabiliana na virusi hivyo.
Hivi sasa, wataalamu wa China na wenzao kutoka Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, na Umoja wa nchi za Asia Kusini Mashariki wamefanya mikutano kwa njia ya video, wakibadilishana uzoefu, na mbinu za China katika kukinga na kutibu ugonjwa huo zimetafsiriwa kwa lugha mbalimbali. Aidha China imelifadhili Shirika la Afya Duniani (WHO), kutoa msaada, kusafirisha vifaa vya kinga na kupeleka timu za wataalamu kwa nchi za nje, na kuanzisha ushirikiano wa kimataifa katika kutafiti dawa, chanjo na vipimo vya virusi vya korona.
Swali ambalo wengi wanajiuliza, ni kwa nini China imefanya hayo yote? Bila shaka ni kutoa shukrani kwa jamii ya kimataifa ambayo iliiunga mkono kithabiti China wakati nchi hiyo ilipokuwa katika hali mbaya ya maambukizi. Lakini pia China imefanya hivyo kwa vile inabeba wajibu wa kulinda usalama wa afya duniani, na inatekeleza kwa vitendo nia ya binadamu ya kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja.
Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na China zimeigwa na nchi nyingine. Kwa mfano serikali ya Italia imechukua hatua za kudhibiti usafiri katika miji mikubwa ya Milan na Venice. Iran, ikisaidiwa na wataalamu wa China, imejenga hospitali maalumu ya muda ya kuwatibu wagonjwa wa COVID-19.
Hivi sasa dunia inakabiliwa na hali ya utata. Mkurugenzi mkuu wa WHO Bw Tedros Ghebreyesus jana alisema, idadi ya watu walioambukizwa COVID-19, vifo, na idadi ya nchi na sehemu zitakazoathiriwa na ugonjwa huo zitaongezeka katika wiki kadhaa zijazo. Kutokana na hilo, amezisihi nchi mbalimbali zibebe wajibu na kuonyesha huruma, ili zishirikiane katika kukabiliana na maambukizi.
Katika wakati huu mgumu, inasikitisha kuona hatua za kutowajibika za baadhi ya nchi. Ikiwa ni nchi yenye nguvu zaidi duniani, Marekani yenyewe imekosa muda mwafaka wa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, na hata ilitangaza kupunguza msaada wa fedha kwa WHO, kukataa kulegeza vikwazo dhidi ya Iran, ambayo inakosa pesa za kununua vifaa na dawa.
Jana jioni Marekani iliulaumu Umoja wa Ulaya kwa kuchelewa kukabiliana na "virusi vya kigeni". Kuhusu kauli hiyo, Shirika la Habari nchini humo CNN linasema, hali mbaya ya maambukizi nchini Marekani inatokana na tatizo la kazi ya kupima virusi, na kuita virusi vya korona kuwa "virusi vya kigeni" ni kutafuta mtu wa kubebeshwa lawama, na serikali ya Marekani inakwepa wajibu wake.
Virusi vya korona ni adui wa pamoja wa binadamu, kwa hiyo mapambano dhidi ya maambukizi hayo yanahitaji mshikamano wa jamii ya kimataifa. Yaliyotokea nchini China yanathibitisha kuwa, maambukizi hayo hakika yanaweza kuzuiliwa. Ni wakati kwa binadamu kushikamana na kufanya vitendo kwa pamoja ili kuokoa maisha.