Chuki dhidi ya China haitasaidia Marekani kushinda vita dhidi ya COVID-19
2020-03-18 17:59:02| CRI

Jumatatu, rais Donald Trump wa Marekani kwenye akaunti yake ya Twitter aliviita virusi vipya vya korona kuwa "virusi vya China", na kusababisha shutuma kali ndani na nje ya nchi hiyo. Wizara ya Mambo ya Nje ya China imeikosoa kauli hiyo, huku mkurugenzi wa Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa Marekani CDC Robert Redfield na meya wa mji wa New York Bill de Blasio wakisema kauli hiyo ya ubaguzi inalenga kuibebesha China lawama ambayo haistahili kwa nia ya kufunika mapungufu katika kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo nchini Marekani.

Hivi sasa majimbo yote nchini Marekani yameripoti kesi za virusi vya korona, na idara mbalimbali za nchi hiyo ikiwemo Wizara ya Ulinzi na Shirika la Usafiri wa Anga NASA pia zimeripoti makumi ya kesi za virusi hivyo. Kwa mujibu wa takwimu mpya za Chuo Kikuu cha John Hopkins cha Marekani, kesi zilizothibitishwa za virusi vya korona zimefikia zaidi ya 4,660. Naye mtaalam mwandamizi wa magonjwa ya kuambukiza wa Marekani Anthony Fauci leo ametabiri kuwa, kilele cha maambukizi kitafika baada ya siku 45 zijazo nchini humo, ambapo katika jimbo pekee la New York, vitanda laki 1.1 vya wagonjwa vitahitajika. Lakini wiki moja iliyopita, mtazamo wa serikali ya Marekani kuhusu virusi vya korona ulikuwa "Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi, virusi vitaondoka. Ukilinganisha na hali ya Marekani, idadi ya vifo vilivyotokana na virusi vya korona katika nchi nyingi ni kubwa kiasi cha kushangaza."

Kutokana na kuhofia kushindwa kudhibiti virusi, wikiendi iliyopita Marekani ilitangaza hali ya dharura kote nchini humo. Shule za sehemu mbalimbali na vituo vya utalii vimefungwa, bidhaa zimeadimika madukani kutokana na watu kununua kwa wingi, na soko la hisa liliporomoka sana kiasi cha kulifanya lisimamishwe mara tatu ndani ya siku nane. Kwa hivyo, bila kujali kuviita virusi vya korona kuwa "virusi vya China" au kushutumu nchi za Ulaya kwa kushindwa kudhibiti virusi na kutangaza hatua ya upande mmoja ya kusimamisha huduma za usafiri kati ya Marekani na nchi hizo, lengo halisi la Marekani la kuzibebesha nchi nyingine lawama ambazo hazistahili, ni kuhamisha hasira za wananchi wa Marekani na nchi yao kuchelewa kuchukua hatua na kukosa uwezo wa kukabiliana na maambukizi. Katika kipindi ambacho rais Trump anatarajiwa kugombea muhula mwingine wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kura za watu zitaamua kama atashinda.

China ni nchi ya kwanza kuripoti kesi ya virusi vya korona, lakini hadi sasa hakuna hitimisho juu ya chimbuko la virusi. Shirika la Afya Duniani WHO limepinga hadharani mara nyingi kitendo cha kuhusisha virusi na nchi au sehemu maalum. Wachina hawajawahi kuuita ugonjwa wa mafua aina ya H1N1 uliolipuka Marekani na kusababisha vifo vya malaki ya watu duniani kuwa "mafua ya kimarekani", na watu wa Afrika nao pia wamekuwa wakivumilia kuhusishwa kwa karibu na ugonjwa wa UKIMWI ulioripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Marekani pia. Wakati mlipuko wa virusi vya korona unaenea katika nchi na sehemu nyingi duniani, kinachohitajika ni mshikamano wala sio mafarakano. Mbali na kufanya vizuri kazi za ndani ya nchi, nchi mbalimbali zinapaswa kushirikiana kupambana na virusi vya korona kwa pamoja. Hadi sasa China imetuma vikosi vya wataalam wa afya kwenda Italia, Iran na Iraq ambazo ni nchi zinazoathiriwa vibaya zaidi, wakibeba makumi ya tani za vifaa vya matibabu. Mbali na kutoa vifaa vya kupima virusi kwa nchi za Afrika ikiwemo Kenya, leo wataalam wa China pia watafanya mkutano kwa njia ya video na maofisa wa serikali na wenzao wa nchi zaidi ya 20 za Afrika, ili kueleza uzoefu wao katika kupambana na virusi.

Chini ya ujumbe huu wa rais Trump wa kuviita virusi vya korona kuwa "virusi vya China", kuna maoni yaliyopendwa na watu zaidi ya laki 2.1, yalizungumzia hofu ya mtoa maoni kutokana na Trump kutumia neno la ubaguzi la 'virusi vya China' kuiongoza nchi ya Marekani kuingia kwenye giza ya chuki isiyo na mwisho. Virusi havina uraia, na kitendo cha kuchafua jina la China sio tu hakiongezi imani ya Wamarekani na serikali kushinda vita dhidi ya virusi, bali pia hakizuii kudidimia kwa uchumi wa nchi. Lakini ni rahisi kuipelekea Marekani kukwama kwenye mizozo ya maambukizi ya virusi na chuki dhidi ya wageni kwa wakati mmoja.