WHO yasema China iko wazi kuhusu hali halisi ya maambukizi ya Corona nchini humo
2020-03-20 16:13:59| CRI

Tangu kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa nimonia inayosababishwa na virusi vipya vya corona COVID-19, baadhi ya wanasiasa na vyombo vya habari vya Marekani vimeilaumu bila ya msingi China kwa kuficha hali halisi ya maambukizi ya ugonjwa huo nchini. Lakini hivi karibuni mjumbe wa Shirika la Afya Duniani WHO nchini China Gauden Galea amesema huu sio ukweli.

Galea amesema tarehe 31 Disemba mwaka jana, siku moja kabla ya China kufunga soko la vyakula vya baharini la Huanan mjini Wuhan, WHO ilipewa notisi isiyo rasmi na China kuhusu ugonjwa huo. Tarehe mosi Januari, shirika hilo liliitisha mkutano kati ya ofisi yake nchini China, ofisi yake ya kikanda na makao makuu yake mjini Geneva kwa njia ya simu, na kuunda kikundi cha kukabiliana na ugonjwa huo, kabla ya kupewa notisi rasmi na China tarehe tatu mwezi huohuo. Tarehe 20 na 21 Januari, wafanyakazi wa ofisi yake nchini China walifanya ukaguzi mjini Wuhan.

Mambo yaliyotajwa na Galea yamedhihirisha kuwa China imetoa taarifa kwa WHO kwa wakati, na kitendo hicho kililiwezesha shirika hilo lichambue na kutathmini ugonjwa huo kwa usahihi, na kutoa tahadhari kwa dunia nzima. Juhudi kubwa zilizofanywa na China ziliifanya iwe mstari wa mbele katika kukinga ugonjwa huo kwa jamii ya kimataifa.

Hivi sasa China imefanikiwa kuzuia uenezi wa maambukiz ya Corona nchini. Tarehe 18, hakukuwa na kesi mpya ya maambukizi hayo mkoani Hubei, ambao ni kitovu cha awali cha mlipuko wa virusi hivyo. Wakati huo huo maambukizi ya ugonjwa huo yanaenea kwa kasi nchini Marekani.

Kabla ya hapo, serikali ya Marekani haikuwajibika vizuri kukabiliana na ugonjwa huo, na haikuchukua hatua kwa haraka katika kuchunguza wagonjwa, na kutoa habari sahihi. Hali hii imewasababisha raia wa nchi hiyo kutojitahadharisha vizuri. Huu ni ukweli usiofichika. Mwanzoni mwa mwezi huu, Kituo cha kukinga na kudhibiti magonjwa cha Marekani kilitangaza kusimamisha kutoa taarifa za idadi ya watu waliopimwa na kuthibitishwa kuambukizwa virusi. Kitendo hicho kinachokiuka kanuni ya uwazi wa habari ni kama kuficha hali halisi ya maambukizi ya ugonjwa, na kukosolewa na watu wa nchi hiyo na nchi za nje.

Kutoka kuficha hali halisi ya maambukizi, hadi kusema virusi vipya vya korona ni "virusi vya China", baadhi ya wanasiasa wa Marekani wamekuwa wasumbufu wa juhudi za pamoja za kukabiliana na Corona duniani.

Hivi sasa dunia inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na virusi hivi, na mshikamano na ushirikiano ndio silaha pekee yenye nguvu zaidi ya kushinda ugonjwa huo.