Bidhaa za China kuwa na virusi ni kauli isiyokuwa na ukweli
2020-03-25 20:16:00| CRI

Baadhi ya watu kutoka nchi za Magharibi wakishirikiana na wanasiasa wa Marekani wanaosema virusi vya Corona ni "virusi vya China", wanaeneza habari zisizo za ukweli kwamba bidhaa za China zina virusi vya Corona, ili kuchochea kususia bidhaa zinazotengenezwa na China.

Ukweli ni kwamba, Shirika la Afya Duniani WHO kwenye tovuti yake limedhihirisha kuwa, virusi vya Corona haviwezi kuenea kupitia bidhaa zinazotengenezwa nchini China. Utafiti wa kisayansi umeonesha kuwa, virusi hivyo vinaweza kuwa hai kwa muda tofauti juu ya vitu tofauti, na vinaweza kuwa hai kwa muda zaidi kwenye plastiki na chuma, ambao ni saa 72. Hata hivyo, watu wenye hila ya kuvuruga China wanapuuza sayansi, na kueneza habari zisizo za kweli ili kuchochea uhasama dhidi ya China.

China ni moja ya nchi yenye uwezo zaidi wa kuzalisha vifaa vya matibabu duniani. Kwa mfano inaweza kutengeneza mask milioni 116 kwa siku, ambayo ni muhimu sana katika kukinga virusi vya Corona. Licha ya matumizi ya ndani, China pia inatoa vifaa hivyo kwa nchi nyingine zinazokumbwa zaidi na virusi vya Corona ikiwemo Italia, Iran, Japan, Pakistan, pamoja na nchi za Afrika ambazo kati yao, nyingi hazina uwezo wa kuzalisha vifaa vya matibabu. Habari zilizotolewa na Shirika la Habari la Bloomberg zinasema, hospitali za nchi mbalimbali duniani ikiwemo Marekani zinajitahidi kununua vifaa vya kupumua kutoka China kadiri ziwezavyo. Wakati huohuo, serikali ya China pia imehimiza makampuni yake kuongeza uzalishaji wa bidhaa nyingine mbalimbali, ili kukidhi mahitaji ya nchi nyingine, ambazo uzalishaji wao umekwama kutokana na maambukizi ya virusi.

Mtafiti wa ngazi ya juu wa Chuo Kikuu cha Yale cha Marekani Stephen Roach amependekeza Marekani kushirikiana na China katika kukabiliana na COVID-19, na kununua vifaa vya matibabu vinavyohitajika kwa haraka kutoka China, ili kuokoa maisha ya wagonjwa wengi.

Lakini baadhi ya wanasiasa wa Marekani hawapendi pendekezo kama hilo, lengo lao ni kutenganisha uchumi wa Marekani na China, na kuvuruga uhusiano kati ya China na nchi nyingine duniani.

Katika miaka ya hivi karibuni, China imezidisha mageuzi na kufungua mlango, na kutoa fursa nyingi za maendeleo kwa nchi nyingine. Rais Xi Jinping wa China hivi karibuni ameahidi kuwa, China inapenda kutoa uzoefu na misaada halisi kwa nchi nyingine, ili kuziunga mkono kukabiliana na COVID-19. Kesho rais Xi atahudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa Kundi la Nchi 20 kupitia njia ya video. Kwa kutumia nafasi hii China itahimiza jamii ya kimataifa kushirikiana kupambana na virusi vya Corona, kukamilisha usimamizi wa kimataifa kwa mambo ya afya, kukabiliana na athari ya virusi hivyo kwa uchumi wa dunia.