Maambukizi ya virusi vya Corona yamesababisha kusimama kwa masoko na matumizi duniani, na pia kuathiri mnyororo wa kimataifa wa ugavi. China ambayo imefanikiwa kudhibiti virusi hivyo, inarejesha utaratibu wa kawaida kwa pande zote, na biashara yake ya kuvuka mipaka inafufua mnyororo wa ugavi duniani.
Hivi karibuni, safari za treni kati ya miji ya China ukiwemo Wuhan na nchi za Ulaya zimerejeshwa, hatua itakayosaidia kufufua masoko ya nchi za Asia na Ulaya yaliyokwama kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona. Matunda kutoka nchi za Umoja wa Asia Kusini Mashariki yanaingia China kupitia njia ya reli, huku bidhaa za China zinazoingia kwenye nchi za Ulaya zikiongezeka kwa haraka.
Takwimu zinaonesha kuwa, katika miezi miwili ya mwanzo ya mwaka huu, thamani ya biashara ya mtandaoni ya kuvuka mipaka katika mikoa ya Hainan na Guangdong iliongezeka kwa asilimia 550, na 33.4 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hiki. Wakati huohuo, mauzo ya bidhaa za nje kwenye tovuti ya Taobao ya Alibaba yaliongezeka kwa asilimia 52 kwa mwezi wa Februari.