Kauli ya kupotosha haiwezi kuficha makosa ya Marekani katika kukabiliana na COVID-19
2020-04-12 19:13:52| CRI

Seneta wa Chama cha Republican cha Marekani Bw. Lindsey O. Graham hivi karibuni alipohojiwa na Shirika la Televisheni la FOX amesema, China inapaswa kuwajibika na vifo vya Wamarekani elfu 16 na kukosa ajira kwa Wamarekani milioni 17 kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Graham amesema badala ya rais Donald Trump, China inapaswa kulaumiwa kwa hali mbaya ya maambukizi ya virusi vya Corona nchini Marekani. Wachambuzi wanaona uchaguzi mkuu utafanyika mwezi Oktoba nchini Marekani, kauli hiyo ya kupotosha ni kwa ajili ya kuficha makosa ya serikali ya nchi hiyo, na kulinda maslahi ya kisiasa ya Chama tawala cha Republican.

Gazeti la The Washington Post la Marekani hivi karibuni lilitoa makala, ikikumbusha mambo yaliyofanywa na serikali ya nchi hiyo katika siku 70 tangu China kutoa tahadhari tarehe 3 Januari hadi rais Trump kutangaza hali ya dharura tarehe 13 Machi. Makala hiyo inasema, tarehe 18 Januari Trump alijadiliana kwa mara ya kwanza na waziri wa afya na huduma za jamii Bw. Alex Azar kuhusu virusi vya Corona, na kuona Bw. Azar alikuwa na wasiwasi usio na haja. Halafu mamlaka ya afya na mamlaka ya bajeti zilikuwa zikigongana kuhusu suala la fedha zinazotumiwa dhidi ya virusi hivyo, mpaka tarehe 6 Machi rais Trump asaini mswada wa kutenga fedha. Lakini imechelewa sana.

Gazeti la The Boston Globe la Marekani tarehe 30 Machi pia ilitoa tahariri kuhusu makosa ya serikali, yakiwemo kutochukua hatua kwa wakati, kuchochea ubaguzi kwa kusema virusi vya Corona ni "virusi vya China", kutohimiza ushirikiano wa kimataifa, na kukataa mapendekezo ya watalaam na njia ya kupima virusi iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani. Tahariri hiyo inasema maumivu na vifo vingi vingeweza kuepukwa.

Wachambuzi wanaona kuwa, wakati wa janga la maambukizi ya virusi hatari, badala ya kuhamisha majukumu kwa nchi nyingine, serikali ya Marekani inapaswa kuwajibika na kuzingatia zaidi ushirikiano wa kimataifa. Kwani virusi havijali mipaka na makabila, na jumuiya ya kimataifa inapaswa kushikamana na kushirikiana zaidi ili kushinda virusi hivyo.