Je, kwa nini kampuni za Marekani zinaongeza uwekezaji nchini China wakati wa janga la COVID-19
2020-04-23 20:45:05| CRI

Ujenzi wa mradi wa Kampuni ya ExxonMobil ya Marekani nchini China wenye thamani ya dola bilioni 10 za Kimarekani ulizinduliwa rasmi jana. Kabla ya hapo, Kampuni ya Walmart ya Marekani ilitangaza kuongeza uwekezaji wa dola milioni 420 za Kimarekani mjini Wuhan, China. Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG) limetoa tahariri inayosema "Je, kwa nini kampuni za Marekani zinaongeza uwekezaji nchini China wakati wa janga la COVID-19".

Tahariri hiyo inasema, baada ya kutokea kwa mlipuko wa virusi vya Corona duniani, baadhi ya wanasiasa wa Marekani wametetea kutenganisha uchumi wa nchi hiyo na China, na kusema serikali ya Marekani italipa hasara ya kampuni zake zitakazoondoka China. Hata hivyo, takwimu zilizotolewa na Shirika la Price Waterhouse Coopers la Marekani zinaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 70 ya kampuni za Marekani nchini China zina uhakika kwamba hazitahamisha shughuli zao kutoka China.

Watafiti wa kiuchumi wa Kampuni ya JP Morgan ya Marekani wanakadiria kuwa, China itakuwa nchi ya kwanza itakayofufua uchumi uliodidimia kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona. Hiyo inatokana na kuwa China ina mfumo kamili wa viwanda, miundombinu bora, rasilimali kubwa ya watu, na soko kubwa mno, ambazo hazitabadilika kutokana na maambukizi ya virusi hivyo.

Tahariri hiyo inasema, mwelekeo mzuri wa maendeleo ya uchumi wa China haujabadilika, na hadhi ya kiuchumi ya China duniani ambayo ni sehemu muhimu ya mnyororo wa uzalishaji, na nchi inayovutia zaidi uwekezaji wa nje pia haijabadilika. Kampuni nyingi za kimataifa zinapendelea kujiunga zaidi na uchumi wa China, ili kupata mafanikio ya pamoja.