Leo ni Siku ya Wafanyakazi Duniani. Kutokana na vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, siku hii ina maana tofauti nchini China kwa mwaka huu. Rais Xi Jinping alisema vita hiyo ni ya kiraia, na kusisitiza kuwa kushinda vita hiyo kunategemea wananchi wote wa China. Toka madaktari waliopambana na virusi kwenye mstari wa mbele zaidi, hadi wafanyakazi wanaosambaza vifurushi, mamilioni ya watu wametoa mchango wao kwa ajili ya kushinda vita hiyo, na hao ni mashujaa kweli.
Katika vita hiyo dhidi ya virusi vya Corona, madaktari zaidi ya elfu 40 kutoka sehemu mbalimbali nchini China walikwenda mkoani Hubei, ambao ni kitovu cha maambukizi ya virusi hivyo, na kutoa msaada wa matibabu. Wafanyakazi na watu wanaojitolea zaidi ya milioni nne walishughulika na kazi ya kukagua afya, na kuwasaidia watu wenye matatizo kwenye maeneo laki 6.5 ya makazi. Wakati huohuo, wafanyakazi wanaosambaza vifurushi pia wametoa mchango mkubwa. Gazeti la Times la Marekani limesema, bila ya watu hao, familia nyingi zingekabiliwa na njaa na ukosefu wa vitu muhimu vinavyohitajika kwa maisha ya kila siku.
Hivi sasa, kutokana na mwelekeo mzuri wa juhudi za kukabiliana na virusi vya Corona, China imeharakisha kurudisha uzalishaji, na Wachina wameanza kurudi kazini. Hadi tarehe 14 mwezi Aprili, asilimia 99 ya makampuni makubwa yamerejesha uzalishaji, na asilimia 94 ya wafanyakazi wao wamerudi kazini. Wakati huohuo asilimia 84 ya makampuni madogo na yenye ukubwa ya kati pia yamerejesha uzalishaji.
Kwa mujibu wa mpango kazi uliowekwa mwaka jana, mwaka huu China itatimiza lengo la kutokomeza umaskini unaokithiri, na kumaliza kujenga jamii yenye maisha bora. Ingawa virusi vya Corona vimeleta changamoto kubwa, lakini Wachina zaidi ya bilioni 1.4 wakishikamana vizuri, watashinda changamoto yoyote.