Wanasiasa wanapaswa kuwaacha wanayansi wafanye kazi yao kutafuta chanzo cha virusi
2020-05-04 19:34:17| CRI

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw Mike Pompeo, jana, alirudia kauli yake kuhusu "kuwepo kwa ushahidi mwingi unaoonyesha virusi vya Corona vilitoka katika maabara mjini Wuhan", akifumbia macho maelezo ya ofisi ya mkurugenzi wa upelelezi ya Marekani kwamba, "virusi vya Corona havikutengenezwa na bidanamu, wala havitokani na kubadilisha jeni"

Bw Pompeo pia aliamua kupuuza maelezo ya wanasayansi wa nchi mbalimbali duniani, wakiwemo wanaotoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Taasisi ya Pasteur ya Ufaransa, Profesa Ian Lipkin wa Chuo Kikuu cha Columbia cha Marekani, ambaye ni maarufu kama msakaji wa virusi, na mtaalamu wa kinga za mwili wa Japani Tasuku Honju, ambao wote wamekubaliana kuwa virusi vya Corona ni janga la kimaumbile.

Hivi karibuni Taasisi ya uchunguzi wa virusi ya Wuhan imekuwa inashambuliwa na wanasiasa wa Marekani. Hali halisi ni kwamba, toka kuanzishwa kwake, wanasayansi kutoka nchi mbalimbali duniani ikiwemo Marekani wamekuwa wakiitembelea taasisi hiyo. Mtaalamu wa taasisi hiyo Bw Yuan Zhiming amewaambia wanahabari kutoka nchi mbalimbali kwamba, taasisi yake haina uwezo wa kubuni na kutengeneza aina mpya ya virusi vya Corona, wala haijawahi kufanya hivyo, na maabara zote za taasisi hiyo zinafanya kazi kwa kufuata kwa makini utaratibu unaotambulika kote duniani.

Kutafuta chanzo cha virusi ni suala la kisayansi, na ni bora wanasiasa wakae kimya na kuwaacha wanayansi wafanye kazi yao ya kitaaluma.

Lakini ripoti iliyotolewa hivi majuzi na tovuti maarufu ya Marekani Buzzfeed, imefichua jinsi wanasiasa wa mrengo wa kulia nchini Mrekani na wanaoichukia China walivyobuni taarifa za virusi vya Corona vilitoka maabara ya Wuhan, kwa lengo la kuelekeza hasira za Wamarekani kutoka kwa serikali yao kwenda China, kwa kuwa hii "inaendana na maslahi ya kisiasa ya viongozi wa Marekani na watiifu wao".

Hadi hivi sasa janga la virusi vya Corona limewaua Wamarekani zaidi ya elfu 66, idadi ambayo imezidi ile ya vifo vya wanajeshi wa nchi hiyo katika vita vya Vietnam.

Katika mwaka huu wa uchaguzi mkuu nchini Marekani, baadhi ya wanasiasa, akiwemo Pompeo, wanahangaika kutunga habari za uongo zinazoipaka matope China kwa kutumia janga hilo. Wakati huo huo wameamua kukaa kimya kuhusu maswali kadhaa nyeti, yakiwemo je, kwa nini Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza ya jeshi la nchi kavu la Marekani ililazimishwa kusimamisha miradi husika ya utafiti mwezi Julai mwaka jana? Je, toka msimu wa ugonjwa wa mafua ulipoanza mwaka jana nchini Marekani, miongoni mwa wagonjwa hao, wangapi kihalisi waliambukizwa virusi vya Corona? Toka lini virusi vya Corona vilianza kuenea katika jamii ya Marekani? Na kwa nini mtaalamu maarufu wa magonjwa ya kuambukiza Profesa Anthony Fauci amezuiliwa kutoa ushahidi bungeni?

Walimwengu wanasubiri kwa hamu majibu ya maswali hayo.