Rais wa Marekani apuuza sayansi katika michezo yake ya kisiasa
2020-05-19 20:07:22| CRI

Kampeni ya urais ya Donald Trump ya mwaka 2016 ilivutia vyama vingi kutokana na chuki yake ya wazi dhidi ya sayansi, ikiwemo nadhari ya kuwa na mashaka juu ya chanjo, na madai yake kuwa mabadiliko ya hali ya hewa ni mzaha ulioanzishwa na China.

Watu wengi hawakufikiri kuwa mtazamo wake huo kuhusu urais ungeendelea na njia hiyo, kwamba atapuuza ufahamu wa wataalam na uzoefu wa kisayansi kwa ajili ya maslahi yake binafsi ya kisiasa. Lakini mgogoro wa sasa wa virusi vya Corona umewadhihirishia kuwa si kweli.

Uamuzi wa hivi karibuni wa utawala wa rais Trump kumwondoa mtaalam wa ngazi ya juu wa masuala ya virusi nchini humo Rick Bright wakati mlipuko wa virusi uko katika kilele, kwa mara nyingine tena umeishtua jamii ya wanasayansi. Bright aliongoza taasisi ya serikali kutengeneza chanjo lakini aliondolewa katika nafasi yake mwezi uliopita kwa sababu alikataa kutangaza dawa inayopendekezwa na rais huyo wa Marekani kuwa inaweza kutumika katika kutibu virusi vya Corona.

Akiongea na waandishi wa habari tarehe 5 mwezi uliopita, rais Trump alisema dawa hiyo ina nguvu sana, lakini haisababishi kifo kwa mtu, na kuongeza kuwa wamepata matokeo mazuri na majaribio yaliyofanikiwa, na kusema hakuna ambacho watapoteza. Lakini utafiti umegundua kuwa, watapoteza maisha yao.

Kutokana na utafiti uliofanywa na Idara ya Afya ya Maveterani nchini Marekani, hydroxychloroquine na kizazi cha chloroquine zimeonyesha kuwa na athari ndogo sana katika kutibu wagonjwa wa virusi vya Corona, na hata inaweza kuongeza hatari ya kifo kwa baadhi ya wagonjwa.

Akitoa ushahidi wake kwenye bunge, Bright alisema alitoa msimamo wake wakati huo, na kama anavyotoa ushahidi wake, kwa sababu ni sayansi, na sio siasa wala urafiki, unaopaswa kuongoza njia ya kukabiliana na virusi hivyo hatari.

Lakini hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa rais Trump kuonyesha kutotilia maanani sayansi. Rais huyo alitumia muda muhimu wa fursa iliyotolewa kupuuza ukubwa wa tatizo la virusi, licha ya mamlaka husika ya masuala ya afya duniani kuonyesha wasiwasi wake juu ya dharura ya afya ya umma. Mwezi Februari, Mkurugenzi wa Idara ya Chanjo na Magonjwa ya Mfumo wa Hewa iliyo chini ya Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa cha Marekani Bi. Nancy Messonnier alitoa tahadhari kwa umma nchini humo, kwamba ni hakika kuwa virusi vitaenea kwa watu wa Marekani. Alisema swali sio kama jambo hilo linaweza kutokea, bali swali halisi ni lini hasa litatokea na watu wangapi nchini humo wataambukizwa virusi hivyo.

Lakini kitu cha kwanza alichofanya rais Trump sio kufikiria kama janga hilo litatokea Marekani, bali ni kukasirishwa na kauli za Bi. Messonnier wakati soko la hisa lilipoanguka. Alimwita Waziri wa Afya na Huduma za Jamii nchini humo Alex Azar na kutishia kumfuta kazi, kwa sababu amewatia hofu Wamarekani bila ya sababu. Kuanzia hapo, Bi. Messonnier ameonekana mara chache sana kwenye mikutano ya waandishi wa habari inayofanyika Ikulu ya Marekani.

Mratibu wa ugonjwa wa Ebola katika utawala wa rais wa zamani wa Marekani Barack Obama, Bw. Ron Klain anasema, rais wa sasa wa Marekani na Ikulu yake wametoa ujumbe wa wazi kwa wanasayansi katika serikali hiyo kuwa, kutakuwa na gharama kwa kuongea ukweli na kutoogopa.

Lakini sio Messonnier pekee anayeongea ukweli. Anthony Fauci, mtaalam wa ngazi ya juu wa magonjwa ya kuambukiza nchini Marekani, naye mara kwa mara amepingana na madai ya rais Trump, na hata wakati mwingine ambapo rais huyo alijaribu kuficha hali halisi ya virusi vya Corona nchini humo. Chuki hiyo ilionekana wazi pale rais Trump alipoandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akitaka Fauci afutwe kazi, baada ya mtaalam huyo kukiri wakati akihojiwa na CNN kuwa kama hatua za kuzuia zingechukuliwa mapema, maisha ya watu wengi yangeokolewa.

Alipotembelea Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa cha Marekani, rais Trump alidai kuwa ana ufahamu mkubwa wa mambo ya kisayansi, jambo lililowashangaza watu wengi. Huenda walishangaa zaidi mwezi mmoja baadaye alipopendekeza kuwachoma watu sindano zenye viuawadudu ili kuua virusi vya Corona, kauli ambayo ililaaniwa vikali na wataalam na jamii ya kimataifa.

Masuala ya kisiasa na kisayansi hayatakiwi kuwa na uadui. Wakikabiliwa na mgogoro, wanasayansi wanatafuta ushahidi na kutoa aina aina zote za kukabiliana nao kwa wanasiasa ili wao waweze kutoa uamuzi wa mwisho. Lakini wanasiasa hawawezi kupuuza ushauri wakati huohuo wakikataa kuwajibika na matokeo yake.

Rais wa Kituo cha Niskanen, Jerry Taylor, ameeleza ni kwa nini sayansi na data halisi haziwezi kuwa na nafasi katika utawala wa rais Trump, akisema wanasayansi wanawaambia mambo yanayowasumbua, kama ni kuhusu E.P.A ama mabadiliko ya hali ya hewa ama virusi vya Corona, utawala wa rais Trump unajihusisha ma mambo ya kufikirika. Rais Trump haamini kwenye mambo magumu, au kwa hakika, hawezi kuuza hadithi ngumu ya janga hili kwa wapiga kura wake, anaweza tu kuuza kujiamini na kulazimisha wakati uchaguzi mkuu ukikaribia.

Lakini matokeo yanaweza kuwa ya kutisha. Wakati rais huyo akiendelea kuwafuta kazi wale wanaopingana naye, Ikulu inazama kwenye mashine yake ya kisiasa inayokandamiza uwezo wa kipekee wa Marekani. Na jibu la kwa nini Marekani haikufanya vizuri katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona linaweza kuwa katika utamaduni wake wa muda mrefu wa kupuuza utaalam wa kisayansi kwa ajili ya sababu za kisiasa.