China yaimarisha imani ya jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na COVID-19
2020-05-19 17:57:16| CRI

Rais Xi Jinping wa China jana alipohutubia ufunguzi wa mkutano wa 73 wa Afya wa Dunia, alijulisha uzoefu wa China katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona, kutoa mapendekezo sita ya kuimarisha juhudi za kupambana na virusi hivyo, na kutangaza hatua tano za kusukuma mbele ushirikiano wa kimataifa. Hotuba hiyo itaimarisha imani ya dunia kushinda virusi hivyo, na kukamilisha mfumo wa usimamizi wa mambo ya kimataifa.

Mapendekezo sita yaliyotolewa na rais Xi ni pamoja na kujitahidi kadiri iwezekanavyo kukinga na kudhibiti COVID-19, kutumia vizuri kazi ya uongozi wa Shirika la Afya Duniani WHO, kuongeza uungaji mkono kwa nchi za Afrika, kuimarisha usimamizi wa mambo ya kiafya duniani, kufufua maendeleo ya uchumi na jamii, na kuongeza ushirikiano wa kimataifa. Mapendekezo hayo yameonesha kuwa, akiwa kiongozi wa nchi kubwa, rais Xi anawajibika na usalama wa afya na maisha ya binadamu. Rais Xi pia amesisitiza kuwa kuzisaidia nchi zinazoendelea haswa nchi za Afrika ni kazi muhimu zaidi kwa sasa. Kauli hiyo inaonesha busara yake ya kutambua vizuri mwelekeo wa maambukizi ya virusi vya Corona duniani. Kama mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Ghebreyesus alivyosema, mwishoni uwezo wa binadamu wa kukabiliana na virusi hivyo unategemea mfumo wa afya wa nchi dhaifu zaidi duniani.

Aidha, kwenye hotuba yake, rais Xi pia ametangaza hatua halisi za China katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona duniani. Hatua hizo ni pamoja na kutoa misaada ya dola bilioni mbili ndani ya miaka miwili, kuanzisha ghala ya kimataifa ya kukabiliana na dharura za kibinadamu nchini China kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, kujenga mfumo wa ushirikiano kati ya hospitali 30 za China na Afrika, kutoa chanjo dhidi ya virusi vya Corona kwa dunia nzima mara itakapokuwa tayari nchini China, na kutekeleza pendekezo la kuahirisha kulipa madeni kwa nchi maskini zaidi kwa kushirikiana na wanachama wengine wa Kundi la Nchi 20.

Hotuba ya rais Xi imepongezwa na jumuiya ya kimataifa. Profesa Noha Bakr wa Chuo Kikuu cha Marekani kilichoko mjini Cairo, Misri amesema, nchi nyingine zinapaswa kujifunza kutoka kwa China, kuunga mkono WHO, kufanya ushirikiano wa kimataifa, na kuzisaidia nchi zinazoendelea kupambana na virusi vya Corona.

Kwenye mkutano huo, mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Ghebreyesus amesema, wakati mshikamano unaposhinda tofauti ya mawazo ya kisiasa, kila kitu kinawezekana. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na viongozi wa nchi mbalimbali pia wameeleza kuunga mkono utaratibu wa pande nyingi na kuongeza uratibu wa ushirikiano katika kukabiliana na virusi vya Corona.

Kutokana na kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona, nchi zote duniani zinapaswa kuacha ubinafsi na uhasama, na kushirikiana na kufanya juhudi za pamoja, ili kushinda virusi hivyo haraka. Kama rais Xi alivyosisitiza mara kwa mara, binadamu iko katika jumuiya yenye hatma ya pamoja, na mshikamano na ushirikiano ni silaha yenye nguvu zaidi ya kushinda virusi vya Corona.