Wanasiasa wa Marekani wanataka kuwa bingwa wa kukwepa wajibu?
2020-05-20 20:20:26| CRI

Rais Donald Trump wa Marekani hivi karibuni kwenye mtandao wa kijamii ameweka barua aliyomwandikia mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO Tedros Ghebreyesus, akitishia kwamba, kama shirika hilo halitafanya mageuzi makubwa ndani ya siku 30, Marekani haitalifadhili tena, na kufikiria kujitoa kwenye shirika hilo. Kuhusu kauli hiyo, Shirika Kuu la Utangazaji la China limetoa tahariri ikiuliza, je, wanasiasa wa Marekani wanataka kuwa bingwa wa kukwepa wajibu.

Tahariri hiyo inasema, kinyume na Marekani, kwenye mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Afya la Dunia uliofungwa jana, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, na viongozi wa nchi mbalimbali zikiwemo China, Ujerumani, Ufaransa wameeleza kuiunga mkono WHO, na kusisitiza kuwa sasa ni wakati wa kushikamana, si wakati wa kulalamika na kuharibu utaratibu wa pande nyingi.

Tahariri hiyo inasema, tangu kutokea kwa mlipuko wa maambukizi ya virusi vya Corona, kutokana na kushindwa kukabiliana na virusi hivyo, baadhi ya wanasiasa na viongozi wa Marekani wamekwepa wajibu wao kwa kuzitupia lawama pande mbalimbali, ikiwemo China, WHO, Umoja wa Ulaya, na hata wapinzani wao wa kisiasa nchini Marekani. Hata hivyo, hawawezi kukwepa kuwajibika kutokana na kufanya makosa mengi katika kukabiliana na virusi vya Corona. Vyombo vya habari vya Marekani vimesema kuwa, serikali ya nchi hiyo ilipuuza tahadhari iliyotolewa mapema na China na WHO, na kukosa fursa nzuri ya kukabiliana na virusi hivyo, makosa hayo ndiyo sababu ya ueneaji mkubwa wa virusi vya Corona nchini humo.