Mikutano miwili mikuu ya kisiasa nchini China ni majukwaa ya kutoa ishara za sera, na pia ni dirisha linalotumiwa na jamii ya kimataifa kutazama nchi hiyo. Katika mikutano hiyo ya mwaka huu, pande nyingi zinafuatilia jinsi China itakavyotimiza malengo ya maendeleo ya uchumi na jamii, haswa lengo la kutokomeza umaskini uliokithiri.
Mlipuko wa maambukizi ya virusi vya Corona uliotokea ghafla hauzuii juhudi za China kutimiza malengo ya maendeleo ya uchumi na jamii. Kutokana na nia imara, hatua madhubuti, na nguvu mpya, China ina imani, mazingira na uwezo wa kutimiza malengo ya maendeleo ya uchumi na jamii kama ilivyopanga.
Kwanza, chama tawala cha China kinashikilia kanuni ya kuzingatia zaidi watu, na kuweka kipaumbele katika juhudi za kuondoa umaskini. Tangu mkutano mkuu wa 18 wa Chama cha Kikomunisti cha China CPC, rais Xi Jinping amejishughulisha na juhudi hizo, na kutoa maelekezo na njia ya kuondoa umaskini. Kwa nyakati tofauti, alitembelea zaidi ya vijiji 20 vilivyokumbwa na umaskini uliokithiri. Amesisitiza kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, kutokomeza umaskini uliokithiri vijijini ni ahadi kuu ya Kamati Kuu ya CPC kwa watu wa China, na ni lazima itimizwe kama ilivyopangwa.
Kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona, kuhakikisha watu maskini wanapata ajira ni jambo muhimu zaidi katika kutimiza lengo hilo. China imetoa sera ya kuwasaidia watu maskini vijijini kupata kazi mijini, na kuwasaidia wale walioshindwa kufanya kazi mijini kupata kazi kwenye maskani zao. Aidha, kwa kutegemea kukua kwa biashara ya mtandaoni, wakulima maskini wengi wameongeza mauzo ya mazao yao ya kilimo.
Mafanikio ya kuondoa umaskini nchini China pia yamenufaisha dunia nzima. Takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia zinaonesha kuwa, mchango wa China kwa kazi ya kuondoa umaskini duniani umezidi asilimia 70. Mtaalamu wa mambo ya kimataifa wa Kenya Adhere Cavince amesema, mafanikio ya China katika kupunguza umaskini ni muujiza katika historia ya binadamu.
Mwenyekiti wa heshima wa Shirikisho la Prussian la mji wa Berlin, Ujerumani, Volker Tschapke hivi karibuni amesema, mlipuko wa virusi vya Corona hautaathiri malengo ya China ya kuondoa umaskini na kujenga jamii yenye maisha bora. Katika mikutano miwili ya kisiasa ya China ya mwaka huu, wajumbe watajadili mambo ya kitaifa kama walivyofanya zamani, na kutoa mapendekezo kwa maendeleo ya uchumi na jamii, na "kufanikiwa kutokomeza umaskini unaokithiri" kutakuwa mwanzo mpya wa Wachina katika mchakato wao wa kuiendeleza nchi yao kwa ushirikiano na mshikamano.