Kudumisha utulivu wa uchumi wa China kusukuma mbele uchumi wa dunia
2020-05-29 10:11:36| CRI

Mkutano wa Bunge la Umma la China ulifungwa jana hapa Beijing. Kwenye mkutano na wanahabari baada ya kufungwa, waziri mkuu wa China Bw. Li Keqiang amefafanua masuala mbalimbali yakiwemo maendeleo ya uchumi wa China, kufungua mlango na ushirikiano, na kuonesha nia thabiti ya China katika kutimiza malengo ya maendeleo ya mwaka huu, kuboresha maisha ya watu na kuchangia maendeleo ya uchumi wa dunia.

Kwenye mkutano huo Bw. Li amejulisha hatua za serikali ya China katika kuhakikisha ajira na maisha ya watu, kusaidia makampuni na kuchochea uhai wao. Hatua hizo zinaonesha busara na nia ya China katika kuendeleza uchumi na kuondoa umaskini unaokithiri. Aidha, maelezo ya Bw. Li kuhusu mapato, ajira na msaada kwa watu wenye matatizo yanaonesha kuwa serikali ya China inazingatia sana maslahi ya watu.

Ikiwa nchi iliyochangia karibu asilimia 30 ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa miaka mingi, China kudumisha utulivu wa uchumi wake baada ya mlipuko wa virusi vya Corona ni mchango mkubwa kwa dunia. Kwenye mkutano huo, China imesisitiza kuwa haitajiendeleza kwa kufunga mlango, na itafungua mlango zaidi na kupanua ushirikiano na dunia. Hali hii inaonesha kuwa, China itaendelea kubeba wajibu na majukumu ya kuhimiza kufufuka kwa uchumi wa dunia kwa kujiendeleza na kufungua mlango zaidi.

Kwenye mkutano huo China pia imesema hivi karibuni jumuiya ya kimataifa inakabiliwa na changamoto za maambukizi ya virusi vya Corona na kudidimika kwa uchumi, ambazo zinapaswa kutatuliwa kwa ushirikiano na mshikamano wa kimataifa. China imesisitiza kuwa uchumi wa China na Marekani unategemeana, kutengana kwa nchi hizo hakutaleta manufaa kwa upande wowote. Katika siku zijazo, China itaendelea kuhimiza kusainiwa kwa Makubaliano ya Uhusiano wa Wenzi wa Kiuchumi wa Kikanda Kwa Pande Zote RCEP mwaka huu, kusukuma mbele ujenzi wa Eneo la Biashara Huria la China, Japan na Korea ya Kusini, na kupenda kujiunga na Makubaliano ya Uhusiano wa Kiwenzi ya Kuvuka Bahari ya Pasifiki CPTPP. Msimamo wa China katika kuhimiza ushirikiano wa kimataifa utasaidia kufufuka kwa uchumi wa dunia.

Kutafuta ushirikiano ili kupata mafanikio ya pamoja kutajinufaisha na kuinufaisha dunia nzima. Kwenye mikutano miwili ya kisiasa ya mwaka huu ya China, hatua mbalimbali zilizochukuliwa na China si kama tu zimeongeza uwezo wa Wachina kushinda changamoto, bali pia zimeimarisha imani ya kufufuka kwa uchumi wa dunia.