Marekani haina haki ya kutetea uhuru wa kutoa maoni kwa vitendo vyake vya kuwatendea vibaya wanahabari
2020-06-03 20:16:05| CRI

Maandamano makubwa kutokana na kuuawa kwa Mmarekani mweusi George Floyd na polisi mzungu yanaendelea nchini Marekani, huku wanahabari wengi wanaoripoti maandamano hayo wakitendewa vibaya na polisi. Shirika Kuu la Utangazaji la China limetoa tahariri ikisema, Marekani haina haki ya kutetea uhuru wa kutoa maoni kutokana na vitendo vyake vya kimabavu dhidi ya wanahabari.

Tahariri hiyo inasema, katika wiki moja iliyopita, matukio mengi ya kimabavu dhidi ya wanahabari yamerekodiwa, wanahabari wamefyatuliwa risasi, wamepigwa, wamepuliziwa maji ya kuwasha na wamekamatwa na polisi. Ofisa mwandamizi wa Shirikisho la Habari za Kidigitali la Radio na Televisheni la Marekani Dan Shelley amesema, vitendo hivyo si kama tu vinawaumiza wanahabari, bali pia vinaumiza watu wote wanaotaka kujua ukweli wa mambo. Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ameonya kuwa, wakati wanahabari wanapolengwa katika mashambulizi, jamii nzima itapata hasara. Hata waziri mkuu wa Australia Scott Morrison ameagiza uchunguzi kwa matukio hayo, na kusema nchi yake iko tayari kufungua mashtaka rasmi.

Tangu awamu hii ya serikali ya Marekani kuingia madarakani, imekuwa kawaida kwao kukandamiza vyombo vya habari. Rais Donald Trump wa nchi hiyo ameweka alama za "habari feki" kwa vyombo vya habari vinavyothubutu kumpinga. Hivi karibuni alizozana na mtandao wa kijamii Twitter, na kutoa amri ya kuiwekea kizuizi. Kwa kuiga vitendo vya kiongozi wao, baadhi ya polisi wa Marekani wameonesha ukatili kwa wanahabari wanaoripoti maandamano. Hali hii inaonesha kuwa Marekani imeacha kabisa madai yake ya kutetea uhuru wa kutoa maoni, na pia imeonesha jaribio la wanasiasa wa nchi hiyo la kuficha ukweli wa mambo.

Tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi vya Corona, serikali ya Marekani imenyima haki ya kutoa maoni ya maofisa na wataalamu wengi wa afya, ambao wanashikilia kuambia ukweli. Wakati huohuo, baadhi ya wanasiasa wa nchi hiyo wanalaumu nchi nyingine kwa kutofuata kanuni ya kulinda uhuru wa kutoa maoni. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo hivi karibuni ameionya China isizuie uhuru wa wanahabari wa Marekani kuripoti kuhusu mambo ya Hong Kong. Lakini labda amesahau kuwa wakati maandamano yakifanyika mkoani Hong Kong, wanahabari wengi kutoka nchi mbalimbali walikuwa mbele ya polisi, na kuripoti kila kilichofanyika. Lakini hivi sasa hakuna wanahabari wanaothubutu kuwa karibu na polisi wa Marekani wakati wa maandamano. Kutokana na kuweka vigezo tofauti, Marekani haina haki ya kutetea uhuru wa kutoa maoni tena.