Eneo la biashara huria la Hainan kuleta fursa mpya kwa maendeleo ya uchumi wa dunia
2020-06-09 09:43:40| CRI

Serikali ya China jana ilifanya mkutano na wanahabari, ikifafanua Mpango wake wa jumla wa Ujenzi wa Eneo la Biashara Huria la Hainan, na kutoa ishara kwamba, wakati mlipuko wa virusi vya Corona unafanya uchumi wa dunia udidimie, na vitendo vya kupinga mafungamano ya uchumi na kujilinda kibiashara vinaongezeka, China itaendelea kufungua mlango, na kushikilia utaratibu wa pande nyingi, ili kuhimiza mafungamano ya uchumi duniani.

Kwa mujibu wa mpango kazi, hadi kufikia mwaka 2025, kwa jumla kiwango cha mazingira ya biashara mkoani Hainan kitakuwa juu zaidi nchini China, na hadi kufikia mwaka 2035, eneo la biashara huria la Hainan litakuwa mfano mpya wa kuigwa kwa uchumi unaofungua mlango nchini China. Mkutano huo umeeleza kuwa, sera za eneo hilo zitakuwa na mfumo kamili, wa kisayansi na wenye ufanisi mkubwa. Mwaka huu, eneo hilo linatarajiwa kutoa orodha ya biashara za huduma za kuvuka mipaka zilizopigwa marufuku, ambayo itakuwa orodha ya kwanza ya aina hiyo nchini China.

Mpango kazi wa ujenzi wa eneo la biashara huria la Hainan unaonesha kuwa, China inajitahidi zaidi kufungua mlango, na licha ya bidhaa na rasilimali za uzalishaji, mchakato huo umeanza kuhusisha taratibu na mifumo ya kibiashara. Vipengele vya sheria ya kuboresha mazingira ya kibiashara vilivyotolewa mwaka 2019 na Baraza la Serikali la China vilifanya sera na hatua za kuboresha mazingira ya kibiashara ziwe vipengele vya sheria. Sheria ya uwekezaji kutoka nje iliyoanza kutekelezwa tarehe mosi Januari mwaka huu imebaini masuala mbalimbali ya kulinda teknolojia na hakimiliki za ubunifu za kampuni za nje, na mfumo wa usimamizi wa orodha ya sekta zilizopigwa marufuku kwa uwekezaji wa nje.

Jambo lingine linalostahili kufuatiliwa ni kwamba, eneo la biashara huria la Hainan linatarajiwa kuhimiza maendeleo ya uchumi wa kikanda na kimataifa. Takwimu zilizotolewa na idara ya takwimu ya mkoa wa Hainan zinaonesha kuwa, katika robo ya kwanza mwaka huu, biashara ya bidhaa kati ya mkoa huo na Umoja wa Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia na nchi za "Ukanda Mmoja, Njia Moja" imeongezeka kwa kasi, na kuchukua asilimia 81.2 ya biashara kati ya mkoa huo na nchi za nje. Mchumi mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Biashara na Uwekezaji wa Kimataifa ya Japan Bw. Noriyoshi Ehara, amesema Hainan ni kitovu cha Asia ya Mashariki na Asia ya Kusini Mashariki, eneo la biashara huria la Hainan linatarajiwa kuwa kituo muhimu cha biashara huria na uchumi uliofungua mlango duniani, na litakuwa kielelezo kwa maendeleo ya uchumi wa dunia.