Marekani yatangaza hali ya hatari kufuatia kufungwa kwa bomba la mafuta baada ya kutokea shambulizi la udukuzi
2021-05-10 16:04:39| Cri

Ikulu ya Marekani jana Jumapili imetangaza hali ya hatari katika majimbo 17 na wilaya ya Columbia, ikiwa ni kujibu hatua ya kufungwa kwa moja ya mabomba makubwa ya mafuta nchini humo.

Tangazo hilo la dharura lililotolewa na Wizara ya Uchukuzi nchini Marekani, linaondoa vizuizi kwa magari na madereva wanaotoa misaada katika maeneo yanayoathiriwa na upungufu wa bidhaa za petrol.

Bomba kuu linalosafirisha mafuta na dizeli katika sehemu ya mashariki na kusini mashariki mwa Marekani limeendelea kufungwa kwa siku mbili baada ya shambulizi la udukuzi kugunduliwa.

Kampuni ya Colonial inayosafirisha mafuta imesema imesitisha kwa muda operesheni zote baada ya kutokea shambulizi la udukuzi Ijumaa iliyopita, na kusema baadhi ya mabomba madogo yanayosafirisha mafuta kati ya kituo hicho na maeneo mengine kwa sasa yanafanya kazi.