Serikali ya Marekani yajiandaa kuchukua hatua zaidi baada ya shambulizi la kimtandao dhidi ya bomba la mafuta
2021-05-11 16:29:29| Cri

Rais wa Marekani, Joe Biden amesema jana kuwa serikali inajiandaa kuchukua hatua zaidi kujibu shambulizi la kimtandao lililotokea kwenye bomba la mafuta la Colonial, ambalo ni bomba kubwa zaidi la kusafirisha bidhaa za mafuta nchini humo.

Akizungumzia kuhusu masuala ya uchumi akiwa Ikulu, rais Biden amesema Wizara ya Nishati inashirikiana moja kwa moja na kampuni ya Colonial ili kuwezesha kurejesha huduma za bomba hilo na kufanya kazi kwa uwezo wake kamili haraka na kwa usalama.

Kauli ya rais Biden imekuja siku chache baada ya Kampuni ya Mafuta ya Colonial kufunga kwa muda operesheni zake zote baada ya shambulizi la kimtandao linalohusisha genge la wahalifu wanaotaka kulipwa.