China yasema Marekani haina nia ya kufanya utafiti wa kisayansi juu ya chanzo cha virusi vya Corona
2021-05-27 19:26:23| Cri

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bw. Zhao Lijian amesema baadhi ya maofisa wa Marekani hawana nia ya kutafuta chanzo cha virusi vya Corona, na kuichafua China kwa kutumia maambukizi ya virusi hivyo.

Rais Joe Biden wa Marekani aliziamuru idara za upelelezi kufanya uchunguzi juu ya chanzo cha virusi, ikiwa ni pamoja na kuchunguza virusi vilitoka kwenye mazingira ya asili au ajali ya maabara.

Bw. Zhao amesema Shirika la Afya Duniani WHO limetoa uamuzi kuwa haiwezekani virusi hivyo kuvuja kutoka kwenye maabara, na hatua ya Marekani imeonesha kuwa inapuuza ukweli halisi na kutokuwa na nia ya kufanya utafiti wa kisayansi.

Pia amesisitiza kuwa China inatumai Marekani itafuata msimamo wa sayansi na kuanzisha ushirikiano na WHO kufanya utafiti juu ya chanzo cha virusi, na kufanya uchunguzi kwa pande zote, kwa uwazi na kufuata ushahidi, ili kutoa mchango kwa ajili ya binadamu kushinda mapambano dhidi ya virusi hivyo, na kukabiliana kwa ufanisi zaidi matukio ya dharura yatakayotokea katika siku za baadaye.