Ujumbe wa WHA waishukuru China kwa kutoa misaada ya kupambana na COVID-19
2021-05-28 09:42:53| CRI

 

 

Ujumbe kutoka Gambia, Namibia na Sierra Leone jana Alhamis uliishukuru China kwenye mkutano unaoendelea wa 74 wa Baraza la Afya Duniani (WHA) kwa misaada yake na kuunga mkono mwitikio wa COVID-19.

Akiongea kwenye mkutano huo kupitia njia ya video, Waziri wa Afya wa Gambia Ahmadou Lamin Samatch amesema China imetuma wataalamu wa afya nchini Gambia mwishoni mwa mwaka 2020 kwa ajili ya kazi ya miezi mitatu kusaidia nchi hiyo kupamabana na COVID-19, halikadhalika wajasiriamali wa China nao pia wamechangia vifaa vya matibabu katika kipindi cha mapema wakati janga linaibuka. Nazo Namibia na Sierra Leone zimeishukuru China kwa kuwa nchi ya kwanza kuchangia chanjo, ambapo Namibia ilipata shehena ya kwanza Machi 17, huku Sierra Leone ikipokea dozi 240,000 za chanjo ya Sinopharm.

Mkutano wa WHA uliendelea Alhamis kwa wajumbe kujadili masuala kama namna ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, matibabu ya saratani na magonjwa yasiyo ya kawaida, hatua za kuchukua kwa usalama wa mgonjwa na usugu wa vijidudu.