Mamlaka ya Upelelezi ya Denmark yashirikiana na Marekani kuwapeleleza washirika wao
2021-06-01 09:31:55| Cri

Shirika la utangazaji la Denmark DR News limeripoti kuwa, Mamlaka ya Upelelezi ya Ulinzi ya Denmark (FE) imelipa Shirika la Usalama la Kitaifa la Marekani NSA mamlaka ya kuingia kwenye mtandao wa Internet ili kuwapeleleza wanasiasa wakuu wa nchi jirani, akiwemo chansela wa Ujerumani Angela Merkel.

DR News, ikishirikiana na vyombo vya habari vya Sweden, Norway, Ujerumani na Ufaransa, vimegundua matokeo ya kushangaza katika uchunguzi wa siri wa ndani kuhusu FE unaoitwa “Operesheni Dunhammer” ambayo ilikamilishwa mwezi Mei mwaka 2015.

Waziri wa Ulinzi wa Denmark Trine Bramsen alijibu ripoti za vyombo vya habari kwa kutuma barua pepe kwa DR News, akisema kuwa serikali “haitaingia katika uvumi kuhusu mambo yoyote ya kijasusi kutoka kwa waandishi wahabari au njia nyingine, kwani kuwapeleleza wenzi ni suala lisilokubalika” .

Lakini serikali za Norway na Sweden zinaishinikiza serikali ya Denmark na kudai majibu ya haraka juu ya vitendo vya upelelezi vya NSA kupitia mkonga wa Denmark.