WHO laidhinisha chanjo ya COVID-19 ya CoronaVac kutoka Kampuni ya Sinovac kwa matumizi ya dharura
2021-06-02 09:17:44| Cri

Shirika la Afya Duniani (WHO) jana Jumanne liliidhinisha chanjo ya COVID-19 ya CoronaVac iliyotengezwa na Kampuni ya dawa ya China Sinovac kwa matumizi ya dharura.

Akitoa tangazo hilo kwenye mkutano na wanahabari Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema chanjo ya CoronaVac imeidhinishwa baada ya kuonekana salama, ina ufanisi na kuwa na ubora mkubwa kufuatia dozi mbili za chanjo hiyo. Zaidi ya hapo Bw. Ghebreyesus amesema chanjo hiyo ni rahisi kuhifadhiwa na kufanya ifae kwenye maeneo yenye rasilimali ndogo.

Naye msaidizi wa Katibu Mkuu wa WHO anayeshughulikia Upatikanaji wa Bidhaa za Afya Mariangela Simao, amesema dunia hivi sasa ina mahitaji makubwa ya chanjo mbalimbali za COVID-19 ili kukabiliana na upatikanaji wa chanjo usio na usawa duniani. Amewataka watengezaji kushiriki kwenye kituo cha COVAX, kueleza yale wanayoyajua, kutoa data na kutoa mchango wao wa kufanya janga lidhibitiwe.

Chanjo ya CoronaVac, iliyotengenezwa na Kampuni ya China Sinovac yenye makao yake Beijing, pia ni chanjo ya virusi vilivyodhoofishwa, kama chanjo nyingine, pamoja na chanjo ya kwanza ya COVID-19 ya China, ya Sinopharm, ambayo iliidhinishwa na WHO mapema mwezi uliopita kwa matumizi ya dharura.

Mbali na chanjo mbili za China, WHO awali iliiorodhesha chanjo ya COVID-19 iliyotengezwa na Pfizer/BioNTech, matoleo mawili ya chanjo ya AstraZeneca/Oxford, chanjo ya Janssen na chanjo ya Moderna kwa matumizi ya dharura.

Kwa mujibu wa Timu ya Wataalamu ya Ushauri wa Mikakati ya WHO juu ya Kinga (SAGE) chanjo ya Sinocav imependekezwa kutumiwa kwa watu wazima wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, kwa kuchanjwa dozi mbili zikipishana kwa wiki mbili hadi nne.

Matokeo ya ufanisi wake yanaonesha kuwa chanjo ya Sinovac inakinga mtu kupata dalili kali za COVID-19 na kulazwa hospitali kwa asilimia 100 ya watu waliofanyiwa utafiti. Hata hivyo watu wachache tu wenye umri wa zaidi ya miaka 60 ndio walishirikishwa kwenye majaribio ya kikliniki, hivyo SAGE imesema ufanisi wa chanjo ya Sinovac unaweza usikadiriwe kwa watu wenye umri huu.

China imeshaamua kutoa dozi milioni 10 za chanjo ya COVID-19 kwenye mpango wa COVAX ili kukidhi mahitaji ya dharura ya nchi zinazoendelea, hatua ambayo ni halisi katika kutimiza ahadi ya kufanya chanjo iwe bidhaa ya umma duniani.

Akihutubia kwenye Mkutano wa 74 wa Baraza la Afya Dunia, mjumbe wa China ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Ofisi ya Mwitikio wa Dharura ya Afya Yang Feng amesema China inaamini kwamba kuhimiza usambazaji na upatikanaji sawa wa chanjo ya COVID-19 duniani ni muhimu katika kuzuia na kudhibiti mlipuko, ambapo imetimiza ahadi yake ya kutoa chanjo ya COVID-19 kama bidhaa ya umma kwa kutoa usaidizi wa kimatibabu kwa nchi 80, kusafirisha chanjo kwenye nchi 43 na kusambaza dozi milioni 300 za chanjo duniani.