Nchi za Ulaya zaitaka Marekani kutoa maelezo juu ya tuhuma za kumpeleleza Merkel
2021-06-02 09:25:12| Cri

Nchi za Ulaya zinazitaka Marekani na Denmark kutoa maelezo juu ya ripoti iliyosema Shirika la ujasusi la Marekani limewapeleleza wanasiasa wakuu wa Ulaya, akiwemo chansela wa Ujerumani Angela Merkel kupitia miundombinu ya Denmark.

Shirika la utangazaji la Denmark DR News Jumapili liliripoti kuwa Mamlaka ya Upelelezi ya Ulinzi ya Denmark (FE) imelipa Shirika la Usalama la Kitaifa la Marekani (NSA) mamlaka ya kuingia kwenye mtandao wa Internet ili kuwapeleleza wanasiasa wakuu wa nchi jirani, zikiwemo Ujerumani, Sweden, Norway na Ufaransa.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa Jumatatu alisema ripoti zote juu ya shughuli za ujasusi za Marekani lazima zifafanuliwe, na kuhimiza Denmark na Marekani zitatue suala hilo kwa uwazi. Chansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema anakubaliana na kauli ya Macron.