Bw. Wang Yi ahudhuria mkutano maalumu wa kuadhimisha miaka 30 ya uhusiano wa mazungumzo kati ya China na ASEAN
2021-06-08 08:48:26| CRI

Mkutano maalumu wa mawaziri wa mambo ya nje wa kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa mazungumzo kati ya China na Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia ASEAN ulifanyika jana Jumatatu mjini Chongqing, magharibi mwa China. Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi na mwenzake wa Ufilipino ambayo ni nchi mratibu wa uhusiano kati ya ASEAN na China Bw. Teodoro Locsin Jr. waliongoza mkutano huo kwa pamoja.

Bw. Wang Yi amesema China na ASEAN zinapaswa kutupia macho miaka 30 ijayo, na kuuinua uhusiano wa sasa kati ya pande hizo mbili kuwa uhusiano wa wenzi wa kimkakati, na kujenga jumuiya iliyo karibu zaidi kati ya China na ASEAN yenye hatma ya pamoja.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za ASEAN wamekipongeza chama cha kikomunisti cha China kwa kutimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, na kusifu mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini China. Wamesema wanapenda kuunganisha mikakati ya maendeleo ya nchi zao na upande wa China, na kusukuma mbele uhusiano kati ya ASEAN na China ufikie kiwango cha juu zaidi.