Waziri Mkuu wa Canada asema tukio la kuigonga kwa gari familia ya waislamu ni tukio la kigaidi
2021-06-09 08:44:55| CRI

Waziri Mkuu wa Canada Bw. Justin Trudeau amesema tukio la kuigonga kwa gari familia ya waislamu lililotokea katika jimbo la Ontario nchini Canada na kusababisha vifo vya watu wanne wa familia hiyo, lilikuwa ni tukio la kigaidi lililochochewa na chuki ya kidini.

Akiongea kwenye bunge la nchi hiyo Bw. Trudeau amesema mauaji hayo hayakuwa ajali, lilikuwa ni shambulizi la kigaidi, na kulilaani vikali tukio hilo. Amesema hilo si tukio pekee la namna hiyo, kuna matukio kadhaa ya vurugu dhidi ya waislam yaliyosababisha vifo.

Polisi wa Canada wamesema kijana mmoja mwenye umri wa miaka 20 aliwalenga kwa makusudi wahanga “kwa sababu ya dini yao ya kiislamu”, na sasa kijana huyo amefunguliwa mashtaka ya mauaji.

Bw. Trudeau amesema matukio kama hayo yanachochewa na “lugha mbaya ya kibaguzi” na “itikadi kali” kwenye mitandao ya kijamii, na ameahidi kuwa serikali itaongeza juhudi zake maradufu ili kukabiliana na matukio kama hayo.