Vikwazo 1,000 vya Marekani dhidi ya Iran kuondolewa na vingine 500 kubaki
2021-06-10 08:36:33| CRI

Baada ya mazungumzo ya raundi tano yaliyofanyika mjini Vienna kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 (JCPOA), makubaliano yamefikiwa kuhusu kuondoa vikwazo 1,000 vya Marekani dhidi ya nchi hiyo, lakini vingine 500 ambavyo havijafikiwa makubaliano vitaendelea kuwepo.

Hayo yamesema kwenye bunge la Iran na mkuu wa ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo hayo Bw. Abbas Araqchi, hata hivyo amesema bado utaratibu wa kuondoa vikwazo hivyo haujafikiwa.

Jumanne waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw. Antony Blinken alisema mamia ya vikwazo dhidi ya Iran vitaendelea kuwepo, hata kama Marekani ikirudi kwenye utekelezaji kamili wa makubaliano ya JCPOA.

Raundi nyingine ya mazungumzo kati ya Iran na nchi tano kwenye makubaliano hayo (Marekani, China, Uingereza, Ufaransa, Russia na Ujerumani ) inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii. Wiki iliyopita Bw. Araqchi alisema anatarajia kuwa raundi hii inayofuata itakuwa ya mwisho na itapelekea kufikiwa kwa makubaliano.