Mafanikio ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai yaleta njia mpya ya ushirikiano wa kikanda
2021-06-16 08:57:07| CRI

 

 

Tarehe 15 Juni ni maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Zhao Lijian amesema, katika miaka 20 iliyopita, Jumuiya hiyo imefanya kazi muhimu za kiujenzi kwa kuhimiza usalama, utulivu, maendeleo na ustawi, na kuleta njia mpya ya ushirikiano wa kikanda.

Zhao amesema, nchi wanachama wa Jumuiya hiyo zinafuata kanuni ya kutofungamana, kutopingana na kutolenga upande wa tatu, zinafanya mawasiliano na uratibu wa karibu katika masuala muhimu ya kikanda na kimataifa, na zinaungana mkono katika masuala muhimu haswa yale yanayohusisha maslahi makuu. Pia nchi hizo zinahimiza ushirikiano katika mambo ya usalama ikiwemo mapambano dhidi ya ugaidi na dawa za kulevya, ulinzi mpakani na usalama wa habari, na zimejenga mifumo ya ushirikiano katika sekta za uchumi na biashara, mawasiliano ya barabara, fedha, kilimo na serikali za mitaa.

Ameongeza kuwa, nchi wanachama wa Jumuiya hiyo pia zimetekeleza miradi ya kunufaishana ya ushirikiano katika mambo ya utamaduni, elimu, utalii, vijana, wanawake na mengineyo.