Utafiti wa Marekani waonyesha kuwa huenda virusi vya Corona vilitokea Amerika ya Kaskazini mapema zaidi
2021-06-17 12:23:43| Cri

Habari zinasema matokeo mapya ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya utafiti wa afya ya Marekani yameonyesha kuwa virusi vya Corona vilitokea mwishoni mwa mwaka 2019 nchini Marekani.

Taasisi hiyo ilifanya utafiti juu ya sampuli za damu za watu zaidi ya elfu 24 wa Marekani zilizokusanywa mwezi Januari, Februari na Machi mwaka jana nchini kote, matokeo yameonyesha kuwa virusi vya Corona vilitokea mwezi Disemba mwaka 2019, muda ambao ni mapema zaidi kwa wiki kadhaa tangu serikali ya Marekani ilipotangaza rasmi kugundua wagonjwa waliothibitishwa nchini tarehe 19 mwezi Januari mwaka 2020. Kabla ya hapo, ripoti iliyotolewa na Kituo cha Kinga na Udhibiti wa Magonjwa cha Marekani pia imeonyesha kuwa virusi vya Corona pengine vilitokea mwezi Disemba mwaka 2019 nchini Marekani.

Utafiti wa Ulaya pia umeonyesha kuwa virusi vya Corona vilitokea mwezi Novemba mwaka 2019 barani Ulaya, wagonjwa walioambukizwa pengine walitokea nchini Uswisi mwezi Novemba mwaka 2019, na virusi hivyo huenda vilianza kusambaa nchini Italia katika majira ya joto ya mwaka 2019.