Rais wa China asema nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania kulinda haki na maslahi ya nchi zinazoendelea
2021-06-22 08:52:52| Cri

Rais Xi Jinping wa China amesema kuwa nchi hiyo iko tayari kushirikiana na Tanzania ili kuimarisha uaminifu wa kisiasa, kuimarisha kuungana mkono, kwa pamoja kulinda haki halali na maslahi ya nchi zinazoendelea, na kutoa mchango chanya katika ujenzi wa jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja.

Rais Xi amesema hayo jana katika mazungumzo kwa njia ya simu na rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Amesema, China iko tayari kuunganisha ujenzi wa Ukanda Mmoja na Njia Moja na utekelezaji wa matokeo ya mkutano wa kilele wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) na mikakati ya maendeleo ya Tanzania, na kupanua ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mawasiliano na utalii.

Kwa upande wake, Rais Samia amesema, Tanzania iko tayari kujifunza uzoefu wa China katika kuondokana na umasikini, na pia kuimarisha mabadilishano na ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara na miundombinu. Pia amesema, Tanzania inasimama na China ili kuendeleza ujenzi wa pamoja wa Ukanda Mmoja na Njia Moja, na itatekeleza kikamilifu matokeo ya mkutano wa kilele wa FOCAC uliofanyika Beijing.