Rais wa China atoa wito wa kutafuta maendeleo makubwa zaidi ya uhusiano kati ya China na Jamhuri ya Kongo
2021-06-22 08:35:32| Cri

Rais Xi Jinping wa China amesema China iko tayari kushirikiana na Jamhuri ya Kongo ili kuimarisha uaminifu wa kisiasa na kubadilishana uzoefu, na kutafuta maendeleo makubwa zaidi ya uhusiano kati ya pande hizo mbili.

Katika mazungumzo ya simu na rais Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Kongo, rais Xi amesema China itajitahidi kupata maendeleo mapya katika ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya pande hizo mbili ili kuwanufaisha zaidi watu wa nchi hizo.

Pia ameeleza kuwa China na Afrika zinapendekeza kwa pamoja “Mpango wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Afrika” kwa jamii ya kimataifa, na kuongeza kuwa, China iko tayari kushirikiana na Jamhuri ya Kongo ili kuzishirikisha nchi nyingi zaidi kuunga mkono maendeleo ya Afrika.

Kwa upande wake, rais Sassou Nguesso amepongeza maadhimisho ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China. Amesema, nchi yake iko tayari kushirikiana na China kuimarisha uhusiano wao wa kirafiki, kujenga Ukanda Mmoja Njia Moja, kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, ili kusukuma mbele ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kongo na China, na kati ya Afrika na China.