China yatoa wito wa upatikanaji wa usawa wa chanjo za COVID-19 duniani
2021-06-23 09:15:47| Cri

Mwakilishi wa kudumu wa China kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Balozi Chen Xu amesema, nchi zote zinapaswa kuchukua hatua halisi katika kuziunga mkono nchi zinazoendelea kupata chanjo za COVID-19 kwa wakati.

Balozi Chen amesema hayo Jumatatu wiki hii kwa niaba ya nchi 63, wakati akizungumza katika mjadala kuhusu virusi vya Corona ulioandaliwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC). Amesema kati ya chanjo bilioni 2.6 zilizotolewa kote duniani, asilimia 0.3 tu zimetolewa kwenye nchi zenye kipato cha chini.

Amesema China pia inatoa wito kwa nchi zenye uwezo kushiriki kwenye ushirikiano wa maendeleo ya kimataifa, na kuzisaidia nchi zinazoendelea kutimiza malengo ya maendeleo endelevu na kupunguza athari mbaya zilizoletwa na janga la Corona.