China yaitaka Marekani kufungua Fort Detrick kwa wataalam wa kimataifa ili ichunguzwe
2021-06-24 09:31:43| Cri

China imeitaka tena Marekani kufungua kituo cha utafiti wa matibabu cha Fort Detrick haraka iwezekanavyo, kuwaruhusu wataalam wa kimataifa kupata taarifa husika, na kutangaza matokeo ya tafiti za maabara zake zaidi ya 200 za baiolojia zilizoenea kote duniani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian amesema hayo jana kwenye mkutano na waandishi wa habari alipozungumzia hoja aliyoitoa mbunge wa Republican kutoka jimbo la Wisconsin Mike Gallagher, kuwa China ilificha ukweli kuhusu virusi vya Corona ili kuepuka kubeba lawama.

Bw. Zhao amesema tangu kuibuka kwa virusi hivyo, China imekuwa wazi na kutoa uzoefu kamili katika kuzuia, kudhibiti, kugundua na kutibu kwa nchi nyingine. Amesema China imepokea wataalamu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) mara mbili, na kutoa ripoti za utafiti wa timu ya pamoja ya China na WHO, hivyo kuchangia katika kutafuta chanzo cha virusi vya Corona duniani, mchango unaotambuliwa na jamii ya kimataifa.