Rais wa China ataka kuwepo kwa uhusiano wa wenzi wa karibu wa BRI
2021-06-24 09:32:09| Cri

Rais Xi Jinping wa China asema nchi yake iko tayari kufanya kazi na pande zote katika kujenga uhusiano wa wenzi wa karibu zaidi wa Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI).

Kwenye ujumbe wake katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Asia na Pasifiki kuhusu Ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, rais Xi amesema pendekezo la BRI alilotoa linalenga kusukuma mbele dhamira ya Njia ya Hariri, kufanya kazi kwa pamoja kujenga jukwaa lililo wazi la ushirikiano, na kutoa motisha mpya kwa ushirikiano na maendeleo kati ya nchi. Kwa mujibu wa rais Xi, katika miaka minane iliyopita, nchi 149 zimesaini makubaliano ya ushirikiano na China chini ya BRI, na wenzi wa ushirikiano wanazidi kuongezeka.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa BRI unafuata kanuni za mashauriano ya kina, mchango wa pamoja na manufaa ya pamoja, kushikilia msingi wa uwazi, maendeleo ya kijani, uadilifu na ushirikiano, na kutekeleza ushirikiano kwa viwanda vya juu, kunufaisha watu na maendeleo endelevu.