WHO yasema kesi za COVID-19 barani Afrika zimeweka historia wakati wimbi la tatu likitokea
2021-06-25 08:22:23| Cri

Idadi ya kesi zilizothibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona barani Afrika imeongezeka kwa kasi isiyotarajiwa wakati bara hilo likikabiliwa na wimbi la tatu la mlipuko huo linalohatarisha miundombinu ya afya.

Hayo yamesemwa jana jijini Nairobi, Kenya, na mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Bi. Matshidiso Moeti. Amesema bara hilo linakabiliwa na ongezeko la kasi la maambukizi ya virusi vya Corona yanayochochewa na kulegezwa kwa hatua za vizuizi, baridi, na uwepo wa aina mpya ya virusi.

Wakati huohuo, Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC) kimesema, bara hilo limepata dozi milioni 61.4 za virusi vya Corona hadi sasa, na kwamba asilimia 1.12 ya idadi ya watu barani Afrika wamepata chanjo kamili.

Takwimu zilizotolewa na Kituo hicho zimeonyesha kuwa, mpaka kufikia jana Alhamis, kesi zilizothibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona barani Afrika ilifikia 5,288,323.