China yakabidhi jengo la kufundishia na ukumbi kwa Chuo Kikuu cha Kabul cha Afghanistan
2021-06-28 09:16:44| cri

China imekabidhi jengo la kufundishia na jengo la ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kabul cha Afghanistan yaliyojengwa kwa msaada wa China. Balozi wa China nchini Afghanistan Wang Yu na mkuu wa Chuo Kikuu cha Kabul Bw. Mohammad Osman Babury, wamesaini hati ya makabidhiano ya majengo hayo.

Akihutubia hafla ya makabidhiano Balozi Wang Yu alisema China inaiunga mkono Afghanistan siku zote katika juhudi zake za kuendeleza miundombinu ikiwemo miradi mingi ya umma, na pia imeisaidia Afghanistan kupambana na janga la virusi vya Corona. China pia itaendelea kuunga mkono mchakato wa kusuluhisha migogoro kwa njia ya amani unaoshirikisha watu na serikali ya Afghanistan pamoja na pande mbalimbali husika za nchi hiyo na kuhimiza ujenzi mpya wa amani ya nchi hiyo.

Bw. Mohammad Osman Babury ameshukuru misaada inayotolewa na China kwa Afghanistan kwa muda mrefu, na kusema chuo chake kitazindua majengo hayo haraka iwezekanavyo na kutumai kuwa nchi hizo mbili zitaimarishe zaidi ushirikiano wa elimu haswa wa elimu ya juu katika siku za mbele.