Mjumbe wa China ahimiza kuwekwa kanuni za usalama mtandaoni zinazokubalika kimataifa
2021-06-30 08:17:07| CRI

Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Balozi Zhang Jun ametoa wito wa kufanywa juhudi kutunga kanuni za kimataifa za usalama wa mtandaoni zinazokubaliwa na nchi zote.

Akiongea kwenye mjadala wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu usalama wa mtandaoni uliofanyika kwa njia ya video, Balozi Zhang Jun amesema nchi zote zinapaswa kushikilia mfumo wenye ufanisi wa kushirikisha pande zote, kujenga mchakato wa usimamizi wa usalama wa mtandaoni ulio wazi, shirikishi na endelevu chini ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, ukiwa na ushiriki sawa wa wote, kutunga kanuni za kimataifa kuhusu usalama wa mtandaoni zinazokubalika kwa nchi zote, na kupinga vikundi vidogo na siasa ya makundi.

Balozi Zhang Jun amesema China iko tayari kushirikiana na pande zote kuendeleza mkataba wa kimataifa dhidi ya uhalifu wa mtandao chini ya mfumo wa Umoja wa Mataifa.