Hongera wanawake wa Afrika Mashariki, lakini kuna ya kujifunza kutoka kwa wanawake wa China
2021-07-08 14:21:32| cri

Hongera wanawake wa Afrika Mashariki, lakini kuna ya kujifunza kutoka kwa wanawake wa China_fororder_VCG41N898695654

Na Fadhili Mpunji

Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu eneo la Afrika Mashariki limeng’ara tena kwenye ramani ya dunia, kwa wanawake wake kuwa kwenye nyadhifa za juu za utawala. Kwanza ni nchini Tanzania ambako rais Samia Suluhu aliapishwa kuwa Rais, na nchi Kenya ambako Bibi Martha Koome alichaguliwa kuwa jaji mkuu wa Kenya, hii ni mbali na Rwanda ambako asilimia 61.3 ya wajumbe wa baraza la chini la bunge la nchi hiyo ni wanawake.

 

Kumekuwa na swali, kama mafanikio haya ni ushindi kwenye mapambano ya ukombozi wa mwanamke, au kama kweli madaraka makubwa kwa wanawake yana maana kuwa kazi ya kumkomboa mwanamke imekwisha. Hii ni kutokana na ukweli kwamba tunapozungumzia ukandamizaji wa mwanamke, bahati mbaya ni kuwa tunajikita zaidi kwenye maeneo machache sana, hasa uchache wao kwenye nafasi za uongozi.

 

Katika nusu karne iliyopita hadhi ya wanawake wa China ilikuwa inafanana kiasi na ile ya wanawake wa Afrika, lakini sasa hali iko tofauti sana. Ingawa wanawake wa China nao wana malalamiko yao, kimsingi ni kuwa wamekombolewa na hadhi yao katika jamii imeinuka sana. Lakini ni kipi kilichofanywa wanawake wa China wakombolewe, na kipi kinaweza kuigwa na wanawake wa Afrika?

 

Moja kati ya mambo muhimu yaliyofanyika ilikuwa ni kuweka sheria za kuondoa mila kandamizi kwa wanawake. Kwa mfano sheria ya ndoa ya mwaka 1980 imepiga marufuku mitala, ndoa za lazima, na imeondoa mkazo wa kumpendelea zaidi mwanaume, na ulinzi umeelekezwa kwa mke na watoto. Sheria hiyo imepitiwa na kufanyiwa mabadiliko mara kadhaa, na kuongeza ulinzi wa mwanamke dhidi ya ukatili na matumizi ya mabavu nyumbani. Kwa hiyo nchini China mila potofu au mila za jadi, sio utetezi tena wa ukandamizaji wa mwanamke.

 

Jambo la pili ambalo China imeweza kufanya vizuri, ni kutoa nafasi sawa ya kuelimisha watoto. Wasichana wa China wana fursa ya kwenda shule sawa na wavulana. Takwimu za mwaka 2019 zinaonyesha kuwa kati ya wanafunzi milioni 48 wa vyuo vikuu, wanafunzi milioni 25 walikuwa ni wanawake, na kati ya wanafunzi milioni 2.86 wa ngazi ya shahada ya pili na kuendelea, wanawake walikuwa milioni 1.45 na wanaume milioni 1.41. Idadi zote mbili zinaonyesha kuwa mtoto wa kike hayuko nyuma kwenye elimu katika ngazi zote. Hali hii sio tu ina manufaa kwa wanawake kwenye soko la ajira, bali pia ina manufaa uwezo wao binafsi. Tatizo kubwa lililoko kwenye nchi za Afrika Mashariki ni kuwa, kwenye shule ya msingi idadi ya wasichana ni kubwa kuliko wavulana, lakini kadiri vidato vinavyoongezeka idadi ya wasichana inapungua. Takwimu za wizara ya Elimu ya Kenya zinaonyesha kuwa ni theluthi moja tu ya wasichana wa Kenya ndio wanaendelea na elimu ya juu, hali hii pia ni sawa na Tanzania ambako ni asilimia 31 ya wasichana hujiunga kidato cha tano.

 

Eneo lingine muhimu ambalo China imepiga hatua ni wanawake sehemu muhimu ya nguvu kazi. Utafiti mmoja uliotangazwa na wizara ya leba ya Marekani, unaonyesha kuwa asilimia 70 ya wanawake wa China ni sehemu ya nguvu kazi ya taifa, idadi ambayo inaongoza duniani kwa hatua nyingi sana hata kuliko nchi za magharibi zilizoendelea. Wanawake kuwa sehemu ya nguvu kazi ina maana kuwa pia wanakuwa na nguvu ya kiuchumi na uhuru wa kiuchumi bila kutegemea wanaume. Hali hii ni tofauti na eneo kubwa la Afrika ambapo ni wanawake wachache wenye uhuru wa kiuchumi, wengi wanategemea waume wao, na hali hii inawafanya wawe chini.

 

Mbali na mchango huo kwenye eneo la nguvu kazi, lakini mchango wa mwanamke kwenye pato la familia ni mkubwa. Utafiti uliofanywa hivi karibuni na wachina waliochaguliwa kwa bahati unaonyesha kuwa kati ya pato la wastani la familia yao kwa mwaka likiwa dola elfu 26, mchango wa mwanamke katika pato hilo ni dola elfu 14, ambalo ni zaidi ya nusu. Bila shaka wanawake wa Afrika wangepewa fursa kama hii, familia nyingi zisingekuwa maskini, na hata pato la taifa lingeongezeka sana.

 

Lakini pia kuna maeneo ambayo baadhi ya nchi za Afrika zimeonekana kufanya vizuri kuliko China. Kwa mfano tukiangalia asilimia ya wanawake kati ya wajasiriamali, tunaweza kuona kuwa Uganda inaongoza duniani ikiwa na asilimia 34.8, ikifuatiwa na Botswana yenye asilimia 34.6. Nchini China wanawake wajasiriamali ni asilimia 30. Lakini kutokana na ukubwa wa uchumi wa China nguvu ya wajasiriamali wanawake wa China ni kubwa zaidi.  

 

Lakini kina dada wa kisasa wa China pia wamekuwa nguvu muhimu ya msukumo wa maendeleo ya vijana wa kiume. Mara nyingi chaguo la kwanza la mwanaume kwa wasichana wa China, ni yule mwenye uwezo wa kiuchumi, yaani awe na nyumba, gari, anayeaminika, anayeweza kujitegemea na anayeweza kutegemewa. Hata kama kijana hana vitu hivi, wanachofanya wasichana ni kuangalia nia thabiti ya kijana wa kiume kuchapa kazi na kuwa na maendeleo. Hili linaweza kuonekana kama ni jambo la ajabu, lakini ukweli ni kwamba linatoa msukumo kwa vijana wa kiume kuwa wachapa kazi.

 

Tukiangalia undani wa ukombozi wa mwanamke tunaweza kuona kuwa ni kazi inayohusisha mambo mengi kama sheria, elimu, uchumi, siasa nk na ni mchakato mgumu na wa muda mrefu. China imejitahidi kuangalia changamoto za wanawake katika pande mbalimbali. Madaraka ya juu kwa wanawake ni ishara nzuri inayoonyesha kubadilika kwa mitazamo sugu ya jadi kwamba mwanamke hawezi au haitakiwi kuwa kiongozi. Itakuwa vizuri sana kukiwa na wanawake wa Afrika watakuwa kwenye nafasi za juu za uchumi, elimu na maeneo mengine mengi, kama ilivyo kwenye nchi zilizotangulia duniani. Hii ni kwa manufaa ya jamii nzima, na sio wanawake peke yao.