Jeshi la Marekani kumaliza majukumu yake nchini Afghanistan mwishoni mwa mwezi Agosti
2021-07-09 08:36:37| CRI

 

Rais Joe Biden wa Marekani amesema jeshi la nchi hiyo litamaliza majukumu yake nchini Afghanistan tarehe 31, Agosti.

Rais Biden amesema, mchakato wa kurudisha wanajeshi wa Marekani kutoka nchini Afghanistan unaendelea kwa utaratibu na kwa kasi. Ameongeza kuwa jukumu la jeshi la Marekani nchini Afghanistan si kujenga nchi hiyo, na limetimiza lengo lake la kupambana na ugaidi, ambapo sasa Waafghanistan wana jukumu la kuamua mustakabali wa nchi yao na jinsi ya kuitawala.

Aidha, rais Biden amesema, Marekani itaendelea kutoa msaada kwa serikali na jeshi la Afghanistan, na kushirikiana na pande husika nchini humo na jamii ya kimataifa ili kutimiza mapatano.

Marekani imetangaza kuondoa wanajeshi wake wote nchini Afghanistan kabla ya tarehe 11 mwezi Septemba. Hivi sasa mashambulizi yanatokea mara kwa mara nchini Afghanistan, na hali ya wasiwasi wa usalama imeongezeka siku hadi siku.