Watu 36 wafariki kwenye moto mkubwa uliotokea katika hospitali ya wagonjwa wa Corona nchini Iraq
2021-07-13 09:16:50| CRI

Shirika la habari la Iraq limeripoti kuwa hospitali ya kuwatibu wagonjwa wa COVID-19 iliyoko kwenye mkoa wa Dhi Qar, kusini mwa Iraq imeteketea kwa moto jana, ambapo watu wasiopungua 36 wamefariki.

Habari zimesema kituo cha karantini kwa wagonjwa wa Corona katika Hospitali ya al-Hussein iliyoko mjini al-Nasiriyah, kilomita 375 kusini mwa mji wa Baghdad kimekumbwa na moto mkubwa jana usiku. Moto huo umeenea kwenye baadhi ya sehemu za kituo hicho, ambapo wazimamoto wamejitahidi kuwaondosha wagonjwa na kuzima moto.

Msemaji wa Idara ya Afya ya mkoa wa Dhi Qar, Ammar al-Zamily amesema moto umedhibitiwa, na watu 36 wamethibitishwa kufa kwenye ajali hiyo, ambapo idara hiyo imetangaza hali ya dharura baada ya moto huo.