Reli ya Kisasa ya SGR yaleta mabadiliko katika sekta ya uchukuzi wa shehena na abiria nchini Kenya
2021-07-13 09:57:42| CRI

Reli ya Kisasa ya SGR yaleta mabadiliko katika sekta ya uchukuzi wa shehena na abiria nchini Kenya_fororder_Reli ya Kisasa ya SGR yaleta mabadiliko katika sekta ya uchukuzi wa shehena na abiria nchini Kenya

Ikiwa ni zaidi ya miaka minne sasa tangu reli ya kisasa ya Mombasa-Nairobi nchini Kenya kuanza kutumika, sekta ya uchukuzi wa shehena na abiria imepata mabadiliko makubwa na kusaidia ukuaji wa uchumi na ajira.

Kufikia sasa, zaidi ya abiria milioni tano wamefaidika na uchukuzi wa bei nafuu. Kuongezeka kwa abiria wanaotumia reli hiyo hasa kuelekea Mombasa pia kumesaidia kukuza sekta ya utalii pwani ya Kenya.

Wakenya waliopata mafunzo kutoka kwa wataalam wa China wamezoea kazi.

David Kimani alijiunga na Afristar inayoendesha huduma za treni miaka minne iliyopita akiwa mwanafunzi.

Baada ya kupokea mafunzo ya hali ya juu, alijiunga na Afristar kama dereva wa treni, safari anayosema imemletea tija na kuboresha Maisha yake.

 “Mara ya kwanza nilikuwa kibarua kuwasiliana na walimu wetu wenye asili ya Kichina. Baada ya kuzoeana na kuelewa lugha mambo yakawa mepesi sana. Hivi sasa tunafanya kazi vizuri sana, nafurahia kazi hii na mapato yake pia yameweza kuniinua kimaisha.” Anasema.

"Nimepitia mchakato wa kuwa dereva msaidizi na sasa mimi nimefuzu kuwa dereva hodari. Mara ya kwanza niliendesha treni ilikuwa mnamo 2017. Hiyo ilikuwa kutoka Mombasa hadi Nairobi. Na baadaye nikawa kiongozi wa kundi la madereva,"Kimani anaongeza.

Naye Harrison Kinyanjui ni Mrakibu Msaidizi, Afristar.

Kazi yake na wenzake ni kuelekeza treni kupitia kwa vituo vyote kati ya Nairobi na Mombasa.

"Kazi yangu na wenzangu ni kutoa maelekezo kwa treni moja kwa moja kutoka kituo cha kuondoka na vituo vyote. Tunatoa maelekezo kuhusu ni treni gani itaondoka, itaondoka saa ngapi, itasimama wapi na mambo kama hayo.  Pia tunaamua treni itasimama kwenye reli gani, kwa muda gani na kupisha treni gani" Anasema Kinyanjui.

Kando na kupunguza muda uliokuwa ukitumiwa na abiria wanaosafiri kutoka Nairobi hadi Mombasa, huduma za treni za Madaraka Express zimepunguza misongamano ya magari  ya mizigo barabarani. Kuanzia mwaka wa 2017 kufikia sasa, treni saba zenye mabogi 752 husafirisha mizigo kila siku kati ya bandari ya Mombasa na mji mkuu Nairobi.

Hatua hii imewasaidia wafanyibiashara kupokea mizigo yao kwa haraka na kwa bei nafuu ikilinganishwa na kutumia matrela.

Bi. Faith Gicheru ni miongoni mwa wahudumu ambao wamenufaika na reli hii moja kwa moja. Si kikazi tu bali pia kupitia utangamano na abiria wengine.

Faith alipokea mafunzo yake kwenye taasisi ya mafunzo ya reli Kenya, RTI.

Sehemu ya masomo yake ilifadhiliwa na China na huu ukawa mwanzo wa ushirikiano mzuri baina yake na Wachina. Kama David Kimani, Faith pia alianza kama mwanafunzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa msimamizi wa wafanyikazi wa treni. “nimekutana na kila aina ya watu.

 “Tumeshuhudia matukio ya kupendeza sana, kuna watu wameandaa sherehe za kuzaliwa ndani ya treni, wengine wamechumbiwa mle tukiona. Hili ni jambo la kupendeza sana, licha ya hayo, wapo wale ambao wametumia huduma zetu wakazipenda na hatimaye kuwa marafiki wa dhati. Nimepata marafiki wengi kutokana na SGR.” Anasema Faith.

Kulingana na kituo cha Takwimu cha Kenya tani milioni 4.42 zilikuwa zimesafirisha kupitia reli hiyo ya kisasa mwaka 2020.

KNBS inasema hii ni ongezeko la tani 257,542 kutoka mwaka uliopita, ikionyesha kuongezeka kwa mahitaji ya huduma ya uchukuzi wa reli licha ya athari mbaya za janga la COVID-19.

Jumla ya mapato kutoka kwa huduma ya usafirishaji mnamo 2020 ilifikia shilingi bilioni 11.54 (karibu dola milioni 105.33).

Mataifa yanayopakana na Kenya kama vile Tanzania,Uganda, Rwanda, Burundi pia yana mipango ya kujenga reli sawia itakayounganishwa na ile ya Kenya ili kufanikisha maendeleo ya kanda ya Afrika Mashariki kwa kurahisisha uchukuzi na biashara.