China yaikosoa vikali Marekani kwa kuhodhi chanjo ya COVID-19
2021-07-16 08:34:01| CRI

China imeikosoa vikali Marekani kwa kuhodhi chanjo dhidi ya virusi vya Corona, na kusema kitendo hiki ambacho si cha kuwajibika kimenyima fursa ya nchi zinazoendelea kupata chanjo hiyo kwa haki na usawa.

Gazeti la The Washington Post la Marekani Jumapili iliyopita lilitoa makala likishutumu Marekani kwa kuhodhi chanjo dhidi ya virusi vya Corona na kusababisha upotevu mkubwa wa chanjo hiyo, na kwamba mamilioni ya chanjo zinakaribia kumaliza muda wake, hali ambayo inatarajiwa kuendelea hadi majira ya mpukutiko. Makala hiyo imesema kosa kubwa linalofanywa na Marekani kwa sasa ni kuangalia tu hali ya maambukizi ya ndani ya nchi, na kupuuza tishio la virusi katika nchi za nje.

Akizungumzia makala hiyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bw. Zhao Lijian amesema hivi sasa virusi vya Corona haswa vile vinavyobadilika vinaendelea kusambaa na kutishia nchi mbalimbali, na vitendo vya kuhodhi na kufuja chanjo ni kama kuua fursa za nchi zinazoendelea kuokoa maisha ya watu. Bw. Zhao amesisitiza kuwa China inaona kuwa chanjo ni bidhaa ya umma duniani na kujitahidi kuhakikisha kuwa inapatikana kwa bei nafuu katika nchi zinazoendelea. China inapenda kutoa chanjo kwa nchi za nje kadiri iwezavyo, kushirikiana na pande mbalimbali kujenga jumuiya ya binadamu yenye afya ya pamoja na kutoa mchango mkubwa katika vita dhidi ya virusi hivyo duniani.