Kiongozi wa Taliban aunga mkono suala la Afghanistan litatuliwe kisiasa
2021-07-19 09:21:32| cri

Kiongozi wa kundi la Taliban nchini Afghanistan Hibatullah Akhundzada alipotoa hotuba ya Siku Kuu ya Idd-al-Adha amesema kundi la Taliban linashikilia msimamo thabiti wa kusuluhisha suala la Afghanistan kwa njia ya kisiasa, na litatumia fursa zote kujenga mfumo wa Kiislamu nchini humo na kufikia amani na usalama.

Amesisitiza kuwa kundi lake linapendelea kuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia, kiuchumi na kisiasa huku akiahidi kwamba hawataruhusu nchi yoyote kutumia ardhi ya Afghanistan kutishia nchi nyingine, na amezitaka nchi za nje zisiingilie mambo ya ndani ya nchi hiyo. Pia ameahidi kuwa Taliban itahakikisha usalama wa balozi za nchi za nje, mashirika ya kibinadamu na wawekezaji wa nje nchini humo.

Majeshi ya Marekani na NATO yameondoka Afghanistan tangu mwezi wa Mei mwaka huu, hivi karibuni ofisa mmoja wa taasisi ya Kiislamu nchini Iran Hossein Akbari alitathmini kuwa kuondoka kwa jeshi la Marekani kutoka Afghanistan kungechukuliwa kama “ushindi mkubwa” kwa nchi za kiislamu. Akaeleza kwamba hali ya kuwepo kwa majeshi ya Marekani nchini humo kwa miaka ishirini na kuondoka kwake kumesababisha ombwe la mamlaka na kuharibu uwiano wa madaraka nchini humo na hivyo kuathiri maendeleo ya Afghanistan.