Kikao cha 44 cha Kamati ya Urithi wa Dunia chapitisha azimio la Fuzhou likisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa
2021-07-19 08:54:30| CRI

Kikao cha 44 cha Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO kimepitisha azimio la Fuzhou likisisitiza tena maana kubwa ya kuhifadhi urithi wa dunia na kuanzisha ushirikiano wa kimataifa na haja ya kufanya juhudi za pamoja kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Naibu waziri wa elimu wa China na mkurugenzi wa kamati ya taifa ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa nchini China na mwenyekiti wa Kikao cha 44 cha Kamati ya Urithi wa Dunia Bw. Tian Xuejun, amesema azimio hilo limeeleza kuwa urithi wa dunia ukiwa hazina ya kiutamaduni na kiasili, umetoa mchango mkubwa katika kuhimiza mawasiliano ya utamaduni, amani ya dunia na maendeleo endelevu, huku likisisitiza tena jukumu la pamoja la binadamu la kukabiliana na changamoto mbalimbali za jadi na zisizo za jadi na kuhifadhi urithi wa dunia.

Azimio hili pia limetoa wito kufanya ushirikiano wa kimataifa wenye ukaribu zaidi chini ya utaratibu wa pande nyingi, kuzidisha uungaji mkono kwa nchi zinazoendelea hasa nchi za Afrika na nchi za visiwa vidogovidogo, na kuimarisha elimu kuhusu urithi wa dunia, utoaji wa ujuzi na matumizi ya teknolojia mpya.