China yasema changamoto kwenye uhusiano kati yake na Marekani zinatokana na baadhi ya wamarekani kuichukulia China kama adui wa kufikirika
2021-07-26 16:03:37| Cri

Naibu waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Xie Feng leo huko Tianjin alipokutana na mwenzake wa Marekani Bi Wendy Sherman ambaye yuko ziarani nchini China, amesema chanzo kikuu cha uhusiano kati ya China na Marekani kudidimia na kukabiliwa na changamoto kubwa ni kwamba baadhi ya watu wa Marekani wanaichukulia China kama adui wa kufikirika.

Amesema watu hao wanaichukulia China kama Japan katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na Umoja wa Kisovieti, huku wakijaribu kuhamisha migongano ya ndani kupitia kuchafua jina la China.

Aidha amesema madai ya Marekani ya kulinda “Utaratibu wa Kimataifa Uliojengwa Juu ya Msingi wa Kanuni” yanalenga kupamba kanuni zake na za nchi kadhaa za kimagharibi kuwa kanuni za kimataifa, ili kukandamiza nchi nyingine.

Ameongeza kuwa hivi sasa dunia nzima inatakiwa kushikamana na kushirikiana. Amesema China inapenda kutendeana na Marekani kwa usawa, huku pande mbili zikiweza kutafuta makubaliano ya pamoja na kuheshimu tofauti.