IMF yakadiria uchumi wa dunia utakua kwa asilimia 6 mwaka 2021
2021-07-28 08:55:48| CRI

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) jana jumanne limetoa ripoti mpya ya Matarajio ya Uchumi wa Dunia, na kudumisha makadirio ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa asilimia 6 mwaka 2021, huku matarajio ya ukuaji huo yakiendelea kubadilika katika nchi mbalimbali tangu makadirio yaliyotolewa mwezi April.

Mchumi mkuu wa IMF Gita Gopinath amesema, uchumi wa dunia unaendelea kufufuka, lakini kuna pengo kubwa linaloongezeka kati ya nchi zilizoendelea na masoko mengi yanayoibuka, na nchi zinazoendelea.

Kutokana na makadirio mapya, matarajio ya ukuaji kwa nchi zilizoendelea kwa mwaka huu yameongezeka kwa asilimia 0.5 na kufikia asilimia 5.6, huku kwa masoko yanayoibuka na nchi zinazoendelea makadirio yao yamepungua kwa asilimia 0.4 na kufikia asilimia 6.3.