China yapenda kuendelea kuchangia ujenzi wa amani nchini Sudan
2021-07-28 09:00:06| cri

 

 

Naibu balozi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Dai Bing amesema, China inapenda kushirikiana na jamii ya kimataifa kuendelea kutoa mchango chanya kwa mchakato wa ujenzi wa amani nchini Sudan.

Balozi Dai amesema hayo kwenye mkutano kuhusu suala la kuondoa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika mkoani Darfur nchini Sudan (UNAMID). Amesema hivi sasa mkoa huo uko katika kipindi muhimu cha mpito kutoka kulinda amani hadi kujenga amani. Baada ya kuondoka kwa kikosi hicho, serikali ya Sudan itabeba jukumu kuu la ulinzi wa raia mkoani Darfur, na Umoja wa Mataifa utaisaidia serikali hiyo kuongeza uwezo wa kuwalinda raia, na kuimarisha usalama.

Amesema China ni moja ya nchi zilizopeleka askari wake kwenye Kikosi hicho mapema zaidi, na imetoa mchango kwa amani na utulivu mkoani Darfur. Amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuongeza uungaji mkono na msaada kwa juhudi za kujenga amani huko Darfur, na kuisaidia Sudan kuimarisha uwezo wa kujiendeleza, kushughulikia vizuri masuala makuu yanayosababisha mgogoro haswa mgawanyo wa ardhi, na kuboresha maisha ya watu.