Mkutano wa utangulizi wa mfumo wa chakula wa Umoja wa Mataifa wamalizika
2021-07-29 08:34:29| CRI

Mkutano wa siku tatu wa utangulizi wa Umoja wa Mataifa kuhusu mifumo ya chakula duniani uliofanyika mjini Rome, Italia umemalizika.

Mkutano huo umezungumzia changamoto za chakula zinazoikabili dunia, na kuweka msingi wa mkutano wa kilele wa chakula utakaofanyika Septemba mwaka huu katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliitisha mkutano huo kama njia ya kutoa tahadhari ya kukabiliana na tatizo linaloongezeka la ukosefu wa usalama wa chakula, hususan katika nchi masikini na zinazoendelea.

Mjumbe maalum wa Katibu mkuu huyo katika mkutano wa mwaka huu wa mifumo ya chakula Bi. Agnes Kalibata, ameliambia Shirika la Habari la China Xinhua kuwa, mkutano wa mwaka huu utasaidia kubadilisha mtazamo wa dunia kuhusu mifumo ya chakula na lishe.