UM yathibitisha kuunga mkono Wizara ya Mambo ya Ndani ya Libya
2021-08-02 09:13:26| cri

Msaidizi wa katibu mkuu na mratibu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL Raisedon Zenenga amethibitisha kuwa Ujumbe huo unaunga mkono vipaumbele vya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Libya.

Zenenga alitoa kauli hiyo Jumapili alipozungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya Khaled Mazen mjini Tripoli. Kwenye mkutano wao, maofisa hawa walijadili vipaumbele vya wizara hiyo na hatua zilizopigwa kwenye masuala ya usalama wa uchaguzi mkuu, kurudisha huduma za polisi na miundombinu pamoja na kuundwa kwa Vikosi vya Polisi vya Pamoja ili kutekeleza makubaliano ya kusimamisha vita.

Tangu kuanguka kwa utawala wa kiongozi wa zamani Muammar Gaddafi mwaka 2011, Libya imekuwa ikishuhudia machafuko na ukosefu wa usalama. Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya iliteuliwa miezi kadhaa iliyopita ili kumaliza mgawanyiko wa kisiasa wa miaka mingi na kuandaa uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.