Marekani kuendelea kuunga mkono jeshi la Afghanistan wakati kundi la Taliban likizidi kusonga mbele
2021-08-10 10:09:52| CRI

Wizara ya ulinzi ya Marekani imesema jeshi la Marekani litaendelea kuunga mkono jeshi la Afghanistan kufuatia wapiganaji wa kundi la Taliban kutwaa miji kadhaa wikiendi iliyopita.

Msemaji wa wizara hiyo John Kirby amesema ni wazi kwamba hali ya usalama ya Afghanistan haina mwelekeo sahihi, na Marekani itaendelea kuwaunga mkono kupitia mashambulizi ya anga kama hali itaruhusu.

Ameongeza kuwa Jeshi la Afghanistan lina uwezo na nguvu ya kupambana na kundi la Taliban, huku akisisitiza kuitaka Kabul kutoa mchango katika uongozi wa kisiasa na kijeshi.  

Kirby amekataa kukisia kama jeshi la Marekani litaendelea kutoa uungaji mkono wa anga kwa jeshi la Afghanistan baada ya Agosti 31 au la, tarehe ambayo rais Joe Biden wa Marekani ameamuru jeshi la Marekani kumaliza majukumu yake nchini Afghanistan.