China yasema Marekani haina sifa ya kutoa maoni yasiyowajibika kuhusu suala la bahari ya kusini ya China
2021-08-10 08:57:50| CRI

Mkuu wa ujumbe wa kudumu wa China katika ofisi za Umoja wa Mataifa Balozi Dai Bing, amesema Marekani haina sifa ya kutoa maoni yasiyowajibika kuhusu suala la bahari ya kusini ya China. Amesema Marekani imezungumzia tena suala hilo, na China inapinga vikali.

Akiongea kwenye mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuhusu mambo ya bahari, balozi Dai Bing amesema kwa sasa kutokana na juhudi za pamoja za China na nchi za ASEAN, hali kwenye eneo la bahari ya China Kusini kwa ujumla ni tulivu, na nchi zote zinafurahia uhuru wa kusafiri baharini na angani, kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Amesema Marekani inajaribu kuleta ukorofi bila sababu, kwa kutuma manowari na ndege za kivita kwenye eneo hilo, ikiwa ni ishara ya uchokozi, na kujaribu wazi kuzichonganisha nchi za kanda hiyo.